Baraza la Madiwani la robo ya nne la Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa limefanyika leo, Agosti 13, 2024, katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri, Baraza hilo, ambalo ni la mwisho kwa mwaka wa Fedha 2023/2024, litatamatika rasmi kesho Agosti 14 baada ya kufanyika uchaguzi wa viongozi wa kamati kwa mwaka 2024/2025, Aidha Baraza hilo limewahusisha Waheshimiwa Madiwani, Wakuu wa Idara na Vitengo, Watendaji wa Kata, pamoja na Wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za Serikali.
Katika Baraza hilo, Waheshimiwa Madiwani wamewasilisha taarifa zinazobainisha mambo mbalimbali ikiwemo mafanikio na changamoto walizokutana nazo kwenye Kata zao, huku wakitoa shukrani kwa Serikali kwa kupeleka huduma muhimu za kijamii kama vile maji, elimu, na afya katika Kata zao, wamesema huduma hizo zimechangia kuboresha maisha ya Wananchi wa Wilaya ya Ruangwa na kuongeza ustawi wa jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Andrew Chikongwe, amewapongeza kwa dhati Idara ya fedha na Halmashauri kwa ujumla kwa kufanikisha ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 94 ya lengo. Amesema hii ni hatua kubwa inayodhihirisha ufanisi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma kwa manufaa ya Wananchi.
Mbali na hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Mwalimu George Mbesigwe, ameahidi kuzifanyia kazi changamoto zote zilizosomwa na Waheshimiwa Madiwani kwenye Baraza, kwa umakini na kwa wakati. Amesisitiza kuwa Halmashauri itaweka kipaumbele katika kuzitatua changamoto hizo ili kuhakikisha kuwa Wananchi wa Ruangwa wanapata huduma bora na maendeleo endelevu.
Ikumbukwe, Mabaraza ya Madiwani ndani ya Halmashauri ni muhimu sana kwa kuwa yanawakilisha sauti za wananchi katika maamuzi ya maendeleo, utungaji wa sera, na usimamizi wa rasilimali za umma. Kupitia Mabaraza hayo, Madiwani hujadili mipango ya maendeleo ya Halmashauri, kuhakikisha kwamba maamuzi yanayofanyika yanazingatia mahitaji na maslahi ya Wananchi. Pia, Mabaraza haya ni chombo muhimu cha uwajibikaji, kwani yanawapa Madiwani fursa ya kusimamia utendaji wa Halmashauri.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa