
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa limekaa leo, tarehe 28 Januari 2026, katika Ukumbi Mkubwa wa Mikutano wa Halmashauri, ambapo Madiwani wa Kata zote 22 wamejadili na kuwasilisha taarifa za maendeleo ya kata zao, zikibainisha mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa miradi.
Mkutano huo wa Baraza umehudhuriwa na wataalamu kutoka Idara/Vitengo mbalimbali vya Halmashauri pamoja na taasisi za umma ambapo wamepata fursa ya kujibu hoja, maswali, na kutoa maelekezo yanayohusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika Kata mbalimbali.
Akijibu hoja za Waheshimiwa Madiwani kuhusu utekelezaji wa miradi na shughuli za maendeleo ngazi ya kata, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Ndg. Ernest Haule, aliweka bayana hatua zinazochukuliwa na Halmashauri ili kuhakikisha malengo ya maendeleo yanatekelezwa kwa ufanisi.
“Tunaendelea kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa malengo ya maendeleo kwa maslahi ya wananchi wetu wote.” Amesema Haule.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, Mhe. Fadhily Bakari Mbwelei, amesema kuwa uwasilishaji wa taarifa za Kata ni nyenzo muhimu ya kupima maendeleo halisi yanayogusa wananchi moja kwa moja. Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Madiwani, wataalamu, na wananchi katika kutatua changamoto zilizopo, na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Aidha, katika mkutano huo Waheshimiwa Madiwani wamesisitiza utekelezaji wa miradi ya maji safi na salama, ujenzi na matengenezo ya barabara, pamoja na kuendelea kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, hatua inayolenga kuimarisha uwajibikaji na usimamizi wa maendeleo ngazi ya kata.
Mkutano huo ni kielelezo cha jitihada za Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa za kuimarisha uwazi, uwajibikaji, na ushirikiano kati ya madiwani, wataalamu, na wananchi, kwa lengo la kuhakikisha miradi ya maendeleo inakidhi mahitaji halisi ya jamii na kutoa matokeo chanya kwa maendeleo endelevu ya kata zote wilayani humo.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa