
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa limekaa leo, tarehe 29 Januari 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri, kujadili na kupitia taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni sehemu ya wajibu wake wa kisheria wa kusimamia rasilimali za umma na utekelezaji wa miradi.
Katika kikao hicho, taarifa za kamati zote za Halmashauri ziliwasilishwa na kujadiliwa, huku Madiwani wakitoa maoni, kuuliza maswali na kupendekeza maboresho kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata zote 22 za Wilaya hiyo.
Awali, akifungua Baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Fadhily Bakari Mbwelei, ameeleza mwelekeo wa uongozi wake kwa kipindi cha miaka mitano, akisisitiza mshikamano kati ya Madiwani na wataalamu wa Halmashauri ili kufanikisha maendeleo kwa wananchi.
Amesema uongozi wake utahakikisha miradi viporo na inayoendelea inatembelewa na kukaguliwa mara kwa mara hadi ikamilike, huku masuala ya michezo, ziara za mafunzo, utekelezaji wa sera na ilani, pamoja na ulinzi na usalama yakipewa kipaumbele. Aidha, amewahimiza viongozi kuepuka utendaji wa mazoea na kuweka mbele maslahi ya wananchi.
Akizungumza katika Baraza hilo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Ndg. Ernest Haule, amesema uongozi utaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa kushirikiana na Madiwani na wadau wengine ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati.
Naye Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, Ndg. Juma Mpanda, amewasilisha salamu za Mbunge, akieleza kuwa anaunga mkono juhudi za Halmashauri katika kusukuma ajenda za maendeleo na kuhimiza ushirikiano kati ya viongozi wa kuchaguliwa na wataalamu wa Serikali.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa