
Walimu wa shule za msingi na sekondari wilayani Ruangwa wamepatiwa mafunzo ya matumizi ya mfumo wa e-Utendaji (WATUMISHI) kwa lengo la kuwawezesha kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu yao ya kazi kwa usahihi na kwa wakati kupitia mfumo wa kielektroniki.
Mafunzo hayo yamefanyika leo, tarehe 27 Januari 2026, katika Ukumbi wa Ofisi za CWT zilizopo Ruangwa Mjini, yakihusisha walimu kutoka shule mbalimbali za Wilaya hiyo, ambapo mwitikio na ushiriki wao umekuwa mkubwa.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Utumishi kutoka Mkoa wa Lindi, Bi. Neema Mrisho Konzo, amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuhakikisha walimu wanaelewa kwa kina hatua za kufanya tathmini (assessment) ya utendaji kazi katika mfumo wa e-Utendaji, sambamba na kuzingatia miongozo na ratiba iliyowekwa na Serikali.
Sambamba na hayo, Bi. Neema amesema kuwa utekelezaji sahihi wa zoezi la tathmini katika mfumo huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha uwajibikaji, ufanisi na uwazi katika utumishi wa umma, hususan katika sekta ya elimu.
“Nafurahi kuona walimu mmejitokeza kwa wingi kushiriki mafunzo haya. Hii inaonesha dhamira yenu ya kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia na kuboresha utendaji kazi wenu wa kila siku,” amesema Bi. Neema.
Kwa upande wake, Kinara wa mafunzo ya mfumo wa e-Utendaji (WATUMISHI), Ndg. Mohamedi Hamisi Mohamedi, amesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia walimu kutatua changamoto mbalimbali ambazo walikuwa wakikumbana nazo katika matumizi ya mfumo huo, hatua itakayo rahisisha zoezi zima la tathimini katika Idara ya Elimu.
Aidha, Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi endelevu za Serikali ya Mkoa wa Lindi kuimarisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika utumishi wa umma, kwa lengo la kuongeza uwajibikaji, uwazi na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya watumishi, hususan walimu, ili kuboresha utoaji wa huduma za elimu kwa jamii.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa