
Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa imeendelea kung’ara kielimu baada ya kuongoza Mkoa wa Lindi katika Matokeo ya Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili (FTNA) Novemba 2025 kwa kupata ufaulu wa asilimia 97.36, kiwango ambacho kimeiweka juu ya Halmashauri zote za Mkoa huo.
Takwimu zinaonesha kuwa kati ya wanafunzi 1,551 waliofanya mtihani huo Ruangwa, wanafunzi 1,510 wamefaulu, hali inayoonesha uimara wa jitihada za walimu, wanafunzi na uongozi wa elimu wilayani humo. Ufaulu huo umeongezeka kutoka asilimia 96.80 mwaka 2024 hadi asilimia 97.36 mwaka 2025, ishara ya mafanikio endelevu katika sekta ya elimu.
Aidha, Ruangwa imefanikiwa kupunguza idadi ya wanafunzi waliopata Daraja la Sifuri hadi kufikia wanafunzi 41 sawa na asilimia 2.64, hatua inayochukuliwa kama mafanikio makubwa ikilinganishwa na baadhi ya halmashauri nyingine ndani ya mkoa. Mafanikio haya yanachangiwa na ufuatiliaji wa karibu wa taaluma na ushirikiano kati ya shule, wazazi na viongozi wa elimu.
Katika ngazi ya shule, baadhi ya shule za sekondari za Ruangwa zimeonekana miongoni mwa shule 10 bora katika Mkoa, hali inayoakisi uwekezaji mzuri katika mazingira ya kufundishia na kujifunzia pamoja na nidhamu ya kitaaluma kwa wanafunzi. Hatua hii imeongeza heshima na ushindani chanya wa kielimu wilayani humo.
Kwa ujumla, mafanikio ya Ruangwa katika FTNA 2025 yanaonesha mwelekeo chanya wa maendeleo ya elimu wilayani humo na yanatarajiwa kuwa chachu ya kuongeza juhudi zaidi ili kufikia ufaulu wa juu zaidi katika mitihani ijayo, sambamba na kuinua ubora wa elimu kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa