Waziri Mkuu Awapongeza Wananchi kwa Ujenzi wa Shule
Posted on: November 20th, 2018
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewapongeza wakazi wa kata ya Nachingwea wilayani Ruangwa kwa kujenga shule ya msingi kwenye kijiji cha Kilimahewa.
“Uamuzi wa kujenga shule ya msingi ni sahihi kwa kuwa huwapunguzia watoto kutembea umbali mrefu na pia utarahisisha mazingira ya kusomea kwa watoto wetu.”
Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo alipotembelea eneo la ujenzi wa shule ya msingi Lugalo na kuwataka waendelee na moyo huo.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli inataka kila mtoto aliyefikia umri wa kwenda shule aanzishwe shule na asome .
Kadhalika, Waziri Mkuu ametaka wananchi hao waweke pembeni itikadi zao za kisiasa na badala yake washirikiane kujenga miradi ya maendeleo kwenye eneo lao.
Nae, Mtendaji wa Kijiji cha Kilimahewa, Majuto Ungulu amesema ujenzi wa shule hiyo uliibuliwa na wakazi wa kijiji hicho, ambacho hakina shule ya msingi.
Majuto amesema watoto wa kijiji hicho wanalazimika kutembea umbali wa kilomita mbili hadi shule la msingi Ruangwa, hivyo ujenzi huo utawawezesha kusoma karibu.
Amesema kwa sasa wameanzia na ujenzi wa vyumba vinane vya madarasa, matundu 18 ya vyoo na ofisi mbili za walimu ambapo jumla yake ni sh. milioni 399.8.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametembelea kituo cha afya cha Mbekenyera na kusema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa na kuwataka wananchi wakitunze.
Amesema kwa sasa wananchi hao hawana sababu ya kulipa nauli kwenda Ruangwa kufuata huduma za vipimo na matibabu katika hospitali ya wilaya.
Ametaja baadhi ya huduma zinazopatikana kwa sasa kwenye kituo cha Afya Mbekenyera ambazo awali hazikuwepo ni upasuaji, maabara, mama na mtoto.
Mapema, Waziri Mkuu alikagua eneo la ujenzi wa kituo cha Polisi Ruangwa, alitembelea mradi wa ujenzi wa Mahakama ya wilaya na kukagua ujenzi wa ofisi ya mkuu wa Wilaya.