Wanawake na vijana wa Wilaya ya Ruangwa wamepata fursa muhimu ya kuelimishwa na kuwezeshwa kupitia Kongamano la Fursa za Mikopo za Kuongeza Thamani ya Zao la Korosho, lililofanyika leo Novemba 18, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa.
Kongamano hilo limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Wilaya ya Ruangwa, NMB Foundation na Rabo Foundation, likiwa na lengo la kuwajengea wanavikundi uelewa wa uchakataji, uzalishaji wenye tija, na usimamizi wa mikopo kwa maendeleo ya kiuchumi.

Akifungua kongamano hilo, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hassan Ngoma, aliweka msisitizo mkubwa katika kuongeza thamani ya korosho kama njia ya kuongeza pato la taifa na kuimarisha uchumi wa kaya.
Amesema mazao yanayozalishwa lazima yaongezwe thamani ili wakulima wanufaike zaidi, akibainisha kuwa mlolongo wa thamani wa korosho umeendelea kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi wa Wilaya na taifa kwa ujumla.
“Mazao yote yanayozalishwa yanapaswa kuongezwa thamani ili wananchi wanufaike zaidi na jasho lao. Uzalishaji hauwezi kukua bila kushirikiana na wadau kama NMB; tunawapongeza kwa kuisaidia serikali kuimarisha uchakataji wa zao la korosho,” amesema Mhe. Ngoma.

Mhe. Ngoma aliwashukuru NMB Foundation pamoja na Rabo Foundation kwa kuwekeza katika mifumo ya uchakataji na utoaji wa mikopo rafiki kwa vikundi vya wanawake na vijana, huku akisisitiza kuwa uzalishaji hauwezi kukua bila ushirikiano wa wadau. Aliwataka wananchi kutumia fursa hizo za mikopo vizuri kwa kuimarisha uzalishaji na biashara zao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Ndg. Rashid Namkulala, aliishukuru NMB kupitia NMB Foundation kwa ushirikiano wao wa karibu na Serikali, ambao umewawezesha wakulima na wanavikundi wa uzalishaji wa korosho.

Alibainisha kuwa korosho ni sehemu muhimu ya pato la taifa, hivyo juhudi za kuongeza uzalishaji na ubunifu zinathaminiwa sana na Halmashauri. Aliongeza kuwa Halmashauri iko tayari kuendelea kutoa ushirikiano wowote utakaohitajika kuhakikisha makundi ya wanawake na vijana yanapata ujuzi, mitaji, elimu ya fedha, mbinu za kuongeza thamani ya mazao, pamoja na mikopo na mafunzo yanayotolewa ili kuongeza uwezo wa wanavikundi kusimamia miradi kwa weledi na kuongeza ushiriki wao katika uchumi wa Wilaya.
Katika kongamano hilo, wanavikundi walipata mafunzo kuhusu namna ya kuongeza thamani ya korosho kupitia uchakataji, uongezaji ubora, upatikanaji wa masoko, pamoja na utunzaji bora wa fedha. Mafunzo hayo yamelenga kuhakikisha rasilimali hizo zinabadilishwa kuwa bidhaa zenye ushindani ndani na nje ya nchi.

Viongozi na wadau hao walisema kuwa fursa za mikopo na mafunzo kwa wanawake na vijana ni muhimu kwa kujenga kizazi kinachojitegemea kiuchumi na kuongeza mchango wa Ruangwa katika uzalishaji wa korosho nchini. Waliwataka wanavikundi kuendelea kuungana, kushirikiana, na kutumia maarifa waliyopewa ili kuongeza tija na kuimarisha maendeleo ya jamii.

Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa