Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa Kushirikiana na Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imetoa nafasi 872 kwa wananchi watakaowania nafasi ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi ambao watatambuliwa kupitia Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii.
Akizungumza katika Kikao na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ruangwa leo tarehe 9, 2024 katika Ofisi ya Mkurugenzi, Afisa Mpango wa Taifa wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii Bi.Orsolina Tolage kutoka Wizara ya Afya, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma amesema kila kitongoji kutakuwa na Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wawili.
"Katika kuhakikisha huduma za Afya zinakuwa karibu zaidi na wananchi Serikali imejipanga ambapo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa tunatarajia kupata Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii 872, wawiliwawili kila kitongoji jinsi ya kiume mmoja na jinsi ya kike mmoja , hivyo wataomba nafasi na watachaguliwa kupitia mikutano ya kijiji au mtaa"amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Frank Chonya ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuweka kipaumbele suala la Afya hasa kwa kuweka Mkakati wa kuwa na Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii katika kata 22, vijiji 90 na vitongoji 436 katika Halmashauri hiyo.
"Naishukuru Serikali kwa kuimarisha miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa na hili suala la Mpango Jumuishi wa Wahudumu Ngazi ya Jamii limekuja katika muda mwafaka hivyo tutashirikiana kuhakikisha uchaguzi wa CHW's unafanyika kwa ufasaha.
Ikumbukwe kuwa Uchaguzi wa kuwachagua Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii katika Halmashauri ya Ruangwa unatarajia kuanza mwezi huu ikiwa ni katika Utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii Uliozinduliwa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango tarehe 31,Januari,2024 na lengo ni kupata Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wapatao 137,294 katika Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa