Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amekagua ukarabati wa majengo unaoendelea kufanyika katika shule ya Msingi Mnacho iliyopo Wilayani Ruangwa Mkoani Lindi.
Shule hii ilianzishwa mwaka 1965 na kabla ya ukarabati kufanyika majengo yake yalikuwa hayapo katika hali nzuri. Mhe. Majaliwa akiwa ni mmoja ya wanafunzi ambao wamesoma hapo mwaka kuanzia mwaka 1970 alipoanza darasa la kwanza hadi la saba. Kutokana na uchakavu wa majengo hayo, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliamua kutafuta wafadhili ambao ndiyo wamesaidia kufanya ukarabati na sasa majengo ya shule yamebadilika.
Baada ya ukaguzi, Mhe. Majaliwa aliongea na viongozi, walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mnacho ambapo alianza kwa kuwapongeza walimu kwa uvumilivu waliouonesha kwa kufanya kazi katika mazingira ya majengo chakavu. Pia aliwapongeza kwa kazi nzuri ya ufundishaji wanayoendelea kuifanya.
Aidha, aliwaeleza kuwa pindi ukarabati huu utakapokamilika shule itakuwa imeimarika na kuwa na mwonekano mzuri. “Najua bado zipo changamoto kwenye upande wa nyumba za walimu ambazo nazo zinahitaji ukarabati, ila niahidi kwamba ukarabati huu ukishakamilika eneo litakalofuata ni ukarabati wa nyumba za walimu kuanzia nyumba namba moja hadi namba tano” alisema Mhe. Majaliwa.
Vilevile aliwasihi wanafunzi kusoma kwa bidi ili wakiwa wakubwa waweze kuja kushika nyadhifa mbalimbali kama yeye au hata zaidi. Pia aliwataka wanafunzi kuwaheshimu walimu wao na kuwa na nidhamu ya hali ya juu.
Kwa upande wa wananchi na viongozi waliokuwepo, Mhe. Majaliwa aliwaeleza kuwa ukarabati huu ni mwanzo wa ndoto aliyonayo ya kuboresha miundombinu ya shule hiyo. Aidha, amewasihi sana viongozi, wananchi na walimu kuwa na ushirikiano ili waweze kufanikiwa kuboresha elimu katika Wilaya nzima ya Ruangwa.
Pia Mhe. Majaliwa amewaomba waendelee kumuombea ili aweze kutimiza ndoto zake alizonazo za kuwa na Ruangwa yenye maendeleo na kuwa hilo litawezekana kama wana Ruangwa wote wataungana na kuwa kitu kimoja.
Ukaguzi huu wa shule aliufanya baada ya kumaliza kushiriki mazishi ya aliyekuwa Diwani wa Kata ya Mnacho, Ndg Daniel Petro Mtawa ambae alifariki kutokana na ugonjwa wa moyo uliopelekea mwili kupooza upande mmoja.
Akiwa msibani aliwaomba watu kuendelea kumuombea marehemu, huku akiwasihi watu wote kujiandaa kama maneno ya mtumishi aliyoyasema ya watu kutenda matendo yaliyo mema yanayompendeza Mungu wakati wapo hapa duniani. “Nawapa pole sana wanafamilia, ndugu, jamaa, marafiki na madiwani kwa msiba huu uliotufika, msiba huu umetugusa sote kwani marehemu ni mtu ambaye tulikuwa tukishirikiana nae katika mambo mengi ya kimaendeleo katika wilaya yetu” alisema Mhe. Majaliwa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa