Mgeni rasmi kwenye semina hiyo amekuwa Mheshimiwa Msoga Matiku Magari, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mheshimiwa Hassan Ngoma, semina imehudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo watu wenye mahitaji maalumu, Maafisa wa Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, pamoja na wawakilishi kutoka idara ya mahakama na jeshi la magereza.
Akizungumza kwenye semina hiyo, Ndugu Matiku amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa makundi maalumu na imeweka mikakati ya kuwasaidia kujikwamua kiuchumi na kijamii. Aidha, amewatia moyo wanajamii hao kuchangamkia fursa za kugombea nafasi za uongozi kwenye Serikali za Mitaa katika uchaguzi wa mwaka huu.
"Wazazi wanapaswa kuwatoa hadharani watoto wenye mahitaji maalumu, kwani Serikali inaendelea kuwekeza katika ujenzi wa shule maalumu na kuboresha huduma kwa kundi hili," amesema Matiku.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa LIDEO, Ndugu Jaafari Murtaza, ameongeza maelezo kuhusu malengo ya asasi hiyo, akibainisha jitihada zao za kuendeleza kituo cha mafunzo ya lugha ya alama kilichopo Ngongo, Lindi. Ameongeza kuwa LIDEO inajihusisha na kutoa fursa za mafunzo na miradi ya kijamii kama vile kilimo na umiliki wa ardhi kwa makundi maalumu.
Naye, Afisa manunuzi kanda ya kusini amesema kuzingatia umuhimu wa makundi maalumu Serikali imezitaka taasisi nunuzi kutenga asilimia 30 % ya bajeti ya ununuzi wa umma kwa makundi maalumu ili kukuza ajira binafsi na ujasiriamali .
Kupitia risala iliyosomwa na Alice Namwembe, LIDEO imeainisha changamoto zinazoikabili asasi hiyo, zikiwemo ukosefu wa wadau wa kuwaunga mkono katika kukamilisha ujenzi wa darasa kwa watu wenye mahitaji maalumu katika Manispaa ya Lindi. Namwembe amependekeza Serikali itenge maeneo maalumu kwa gharama nafuu ili kusaidia makundi hayo kumiliki ardhi na kukuza ustawi wao
Kwa ujumla, semina kama hizi ni muhimu katika kuimarisha ushirikishwaji wa makundi maalumu kwenye shughuli za maendeleo, hatua iliyokuwa ikikosekana kwa muda mrefu. Hivi sasa, jitihada za Serikali na asasi kama LIDEO zinaonekana kuwa na matokeo chanya, lakini changamoto za miundombinu na upungufu wa wadau bado zinahitaji kushughulikiwa. Ikiwa mipango madhubuti itawekwa, mustakabali wa makundi maalumu unaweza kuwa wenye matumaini zaidi, kwa kuhakikisha wanapata nafasi sawa za kushiriki katika kila nyanja ya maendeleo.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa