Baraza la Madiwani la Wilaya ya Ruangwa limekutana leo, Novemba 6, 2024, kujadili taarifa za maendeleo na changamoto zilizojitokeza katika Kata zote 22 za Wilaya hiyo kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025, Kikao hicho, kimefanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, kikilenga kuboresha utekelezaji wa miradi na huduma kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Andrew Chikongwe, amewataka Madiwani na Watendaji Kata kusimamia kwa ufanisi ukusanyaji wa mapato ili kukuza uchumi wa Wilaya, Mkoa, na Taifa kwa ujumla. Aidha, amesisitiza umuhimu wa matumizi bora ya rasilimali kwa maendeleo ya wananchi.
Sambamba na hayo, Mhe. Chikongwe pia ametoa wito kwa Maafisa kilimo kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora na kuhamasisha kilimo cha kisasa chenye tija kwa wakulima.
“Twendeni tukawahamasishe wananchi kufanya kilimo cha kisasa chenye tija ili kuongeza vipato vyao,” amesema Mhe. Chikongwe.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Ndugu Frank Fabian Chonya, amepongeza mafanikio yaliyopatikana katika Wilaya kupitia juhudi za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na mchango wa Mbunge wa Ruangwa ambaye ni Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa.
“Mafanikio yapo mengi kuliko changamoto, na hii inaonesha namna Serikali inavyowajibika kutuletea maendeleo Ruangwa, sisi tunashukru sana kwa kila hatua tunayopiga katika Wilaya yetu tunatambua namna Serikali inavyofanya kazi nzuri kwa Wananchi wake usiku na mchana ili kuhakikisha maendeleo yanafika kila sehemu,” amesema Chonya.
Ikumbukwe, Kikao hicho cha Baraza la Madiwani kimeweka msingi thabiti wa ushirikiano na uwajibikaji katika kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Ruangwa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa