Watumishi ajira mpya wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa wamepatiwa mafunzo ya TEHAMA kuhusu usimamizi wa taarifa za kiutumishi, hifadhi ya jamii na huduma za kifedha ili kuongeza ufanisi, uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Mafunzo hayo yamefanyika Novemba 08, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, yakiratibiwa na Idara ya Utumishi kwa kushirikiana na mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja na taasisi za kifedha. Lengo la mafunzo ni kuwawezesha watumishi ajira mpya kutumia kwa ufasaha mfumo wa Public Employees Performance Management Information System (PEPMIS) na kusimamia taarifa zao za kiutumishi kwa usahihi na uwazi.

Aidha, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ruangwa, Ndg. Frank Chonya, amesema Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya TEHAMA ili kuimarisha utendaji wa watumishi wa umma. Ameeleza kuwa matumizi sahihi ya mifumo hiyo yataongeza uwajibikaji, kuimarisha nidhamu kazini na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi. Amesisitiza kuwa kila mtumishi anatakiwa kuelewa na kutumia mfumo ESS-Utumishi ipasavyo ili kuleta matokeo chanya kazini.
Vilevile, Afisa Utumishi wa Halmashauri, Bi. Yasinta Lupenza, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kuhusu usimamizi wa watumishi kwa kutumia mifumo ya kisasa. Alibainisha kuwa uelewa wa mifumo ya TEHAMA husaidia kupunguza ucheleweshaji wa taarifa, kuondoa makosa ya kiutawala na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

Kwa upande mwingine, watumishi ajira mpya waliopata mafunzo hayo wameishukuru Halmashauri kwa kuwapatia elimu hiyo ya awali ya utumishi. Wamesema mafunzo yamewapa msingi thabiti kuhusu uadilifu wa kazi, umuhimu wa kuchangia hifadhi ya jamii na matumizi salama ya huduma za kifedha, hatua ambayo itawawezesha kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kwa ujumla, mafunzo hayo yamehitimishwa kwa kuwataka watumishi kuendelea kujifunza, kuzingatia maadili ya kazi, kufuata kanuni za kiutumishi na kuwa mfano wa uwajibikaji katika maeneo yao ya utumishi ili kuchochea maendeleo ya Ruangwa na Taifa kwa ujumla.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa