Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, Alfed Luanda ameagiza Maafisa Habari na wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Halmashauri na mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma Kuhudhuria mafunzo ya Uimarishaji wa Sekta za Umma yanayoendelea katika ukumbi wa Tiffany Diamond Hotel ulioko mjini Mtwara.
Agizo hilo amelitoa juzi baada ya kutoridhishwa na mahudhurio ya wajumbe wa mafunzo hayo yanayodhaminiwa na USAID kupitia program ya PS3. Amesema Maafisa Habari na wataalam wa TEHAMA wa Mikoa hii mitatu wahakikishe wanawasiliana na Makatibu Tawala wa Mikoa yao ili wanamafunzo ambao hawajafika wafike haraka iwezekanavyo.
Amesisitiza kuwa mafunzo haya yaliyokusudiwa kwa Maafisa Habari na TEHAMA wa mikoa hii mitatu yanapaswa kuwa hamasa kwa walengwa na kuiona kama fursa muhimu yenye lengo la kuwainua kitaaluma. Anasema haitapendekeza kama mradi utamaliza muda wake wakawepo wanufaika wengine ambao hawakuichangamukia fursa hii.
Aidha, Luanda amewatahadharisha wanamafunzo kuhakikisha wanahuisha tovuti zao mara kwa mara bila kusubiri kukumbushwa. Amesema mara nyingi tovuti zimekuwa zikianzishwa pasipo kuendelezwa hivyo huu ni muda muafaka kuhakikisha mafunzo haya yanawajenga katika maarifa ya kwenda na wakati hasa katika kipindi hiki ambacho serikali inasisitiza suala la utendaji kazi uliotukuka.
Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mkuu wa timu ya wawezeshaji, Edgar Mdemu amesema mafunzo haya yanadhaminiwa na USAID na kwamba lengo lake ni kuhakikisha kila Afisa Habari na Mtaalamu wa TEHAMA wa halmashauri na mkoa ulioko katika mradi huo anapata mafunzo kisha kufungua Tovuti ambazo zitazinduliwa rasmi na Waziri wa Habari Utamaduni na Sanaa mjini Dodoma.
Kwa upande wake, Joseline Chambasi, Afisa Habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala amesema mafunzo hayo yatarahisisha utoaji wa taarifa kwani yanaenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia. Amesema dunia ya sasa iko kiganjani tofauti na dunia, hivyo afisa habari anapaswa kuhakikisha anampa mwananchi taarifa kiganjani kwake kupitia teknolojia ya Wakati husika.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa