Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Zainab Athuman Katimba, amefungua mashindano ya SHIMISEMITA Taifa leo 23 Agosti 2025, katika Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga, ambapo Halmashauri 150 kati ya 184 zimehudhuria.
Ufunguzi huo umehudhuriwa na maelfu ya watumishi pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, mashirika na taasisi binafsi. Tukio hilo limeashiria mshikamano mkubwa miongoni mwa watumishi wa umma, huku michezo ikipewa nafasi ya kipekee katika kujenga afya, mshikamano kazini na utulivu wa akili.
Aidha, akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Katimba amesisitiza umuhimu wa watumishi wa umma kushiriki kikamilifu mashindano hayo. Amesema michezo ni nguzo muhimu katika kujenga mshikamo wa kijamii na kudumisha utamaduni wa Kitanzania.
Vilevile, Naibu Waziri huyo amewaagiza Makatibu Tawala na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kurejea maagizo yaliyotolewa awali kuhakikisha michezo na utamaduni vinapewa nafasi ya kipaumbele katika maeneo ya kazi. Amesisitiza kuwa mashindano hayo si burudani pekee bali pia chachu ya mshikamano na afya bora.
Zaidi ya hapo, ameelekeza Halmashauri ambazo bado hazijawaleta watumishi kushiriki mashindano hayo kufanya hivyo ndani ya wiki moja. Ameonya kuwa ushiriki wa watumishi wote ni wajibu na si hiari, kwani mashindano hayo ni sehemu ya kukuza mshikamano na nidhamu ya kikazi.
Sambamba na hilo, Mhe. Katimba amezitaka Halmashauri zote nchini kutenga bajeti maalum kwa ajili ya kuimarisha vitengo vya michezo na utamaduni. Amesema hatua hiyo itahakikisha mashindano ya SHIMISEMITA yanafanyika kwa ufanisi na kuwanufaisha watumishi wote.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa SHIMISEMITA Taifa, Ndugu Jeshi Lupembe, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa ushirikiano mkubwa. Ameeleza kuwa mashindano ya SHIMISEMITA yanatoa fursa ya kujenga mshikamano, kudumisha afya bora kwa watumishi na kukuza ari ya kitaifa.
Ikumbukwe, Kauli mbiu ya mashindano ya mwaka huu ni “Jitokeze Kupiga Kura kwa Maendeleo ya Michezo”, ikisisitiza wajibu wa kila mshiriki na taasisi kuhakikisha michezo inabaki kuwa chachu ya mshikamano na maendeleo ya taifa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa