Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mheshimiwa Hassan Ngoma, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyabiashara Wilaya ya Ruangwa, ameongoza kikao cha baraza hilo leo, tarehe 18 Novemba 2024, katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya.
Kikao hicho kimehusisha viongozi wa wafanyabiashara na wadau wengine muhimu kutoka makundi mbalimbali, wakijadili masuala ya biashara na maendeleo katika Wilaya ya Ruangwa, hata hivyo Kikao cha Baraza la Wafanyabiashara Wilaya ya Ruangwa kimekuwa jukwaa muhimu la kujadili changamoto zinazowakabili wafanyabiashara, kubuni mbinu za kuboresha mazingira ya biashara, na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Wilaya hiyo.
Aidha, Wakati wa kikao hicho, Mh. Ngoma ametumia fursa hiyo kuhimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024.
Katika hotuba yake, Mh. Ngoma amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, huru, na utulivu, akitoa wito kwa wananchi kutanguliza mshikamano na heshima wakati wa mchakato wa uchaguzi.
“Kupiga kura ni kitendo cha siku moja. Itakapofika saa 12:00 jioni ya tarehe 27 Novemba mwaka huu, kila kitu kitakuwa bayana mshindi atajulikana na atakayeshindwa atajulikana. Kwa hiyo, chochote utakachokifanya, kiwe cha kheri na si kuacha makovu kwenye mioyo ya watu,” amesema.
Mbali na hayo, Mhe. Ngoma amewakumbusha wananchi kwamba uchaguzi ni tukio la muda mfupi, lakini maisha ya kijamii yataendelea baada ya uchaguzi, hivyo kuwataka kuzingatia ustawi wa jamii na kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani.
“Uchaguzi utaisha, lakini sisi tunaendelea kuishi pamoja. Endapo utasababisha madhara kwa mtu au familia, utamtazamaje baada ya uchaguzi?” ameongeza Mh. Ngoma kwa kusisitiza mshikamano wa kijamii.
Kikao cha Baraza la Wafanyabiashara kimehitimishwa kwa maazimio yanayolenga kuboresha mazingira ya biashara na kukuza uchumi wa Wilaya ya Ruangwa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa