Kwa sauti za nyundo, mitambo midogo ya uchimbaji, na vumbi linalobeba ahadi za kesho, Ruangwa imegeuka kitovu cha matumaini mapya ya kiuchumi.
Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi, inazidi kung’aa kama almasi mpya kwenye ramani ya madini Tanzania. Kwa miaka mingi, Wilaya hii ilijulikana zaidi kwa kilimo cha korosho, ufugaji na misitu, lakini leo imegeuka kuwa kitovu muhimu cha Wilaya zinazoshikilia nafasi katika utajiri wa rasilimali za madini.
Masikani ya Utajiri Uliolala Chini ya Ardhi
Tafiti mbalimbali pamoja na shughuli za uchimbaji zinaonesha uwepo wa madini yenye thamani kubwa, ikiwemo graphite, dhahabu, shaba, blue sapphire, garnet (nyekundu na kijani), green tourmaline, chrysolite/greenstones, marble nyeupe, pamoja na madini ya ujenzi kama mawe, mchanga na kokoto.
Maeneo kama Mihewe, Mtondo, Nambilanje, Matambarale, Nangurugai, Nachiungo, Namakuku, Namkonjera, Chunyu, Namungo, Kitandi na Nkowe, yamekuwa kivutio cha wawekezaji, wachimbaji wadogo, na makampuni ya utafiti wa kijiolojia, kutokana na utajiri mkubwa wa madini unaopatikana katika maeneo haya.
Fursa Zinazofungua Ajira na Maendeleo
Kila shimo linalochimbwa linabeba tumaini jipya kwa familia zinazohusiana na sekta hii. Uchimbaji wa madini umekuwa chanzo cha ajira kwa vijana na wanawake, kichocheo cha biashara ndogo ndogo, njia ya kuongeza mapato ya Halmashauri, na nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi wa ndani.
Kupitia uongozi thabiti wa Mkuu wa Wilaya, Mhe. Hassan Ngoma, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ndg. Frank Chonya na usimamizi wa kitaalamu wa Ofisi ya Madini Mkoa wa Lindi, Serikali imeweka mazingira rafiki kwa wachimbaji na wawekezaji. Hii inajumuisha kusimamia leseni, kuelimisha wachimbaji kuhusu usalama kazini, kudhibiti uharibifu wa mazingira, na kukuza uwekezaji wenye tija.
Maendeleo Yenye Uwiano na Mazingira
Ruangwa imejifunza kuwa maendeleo ya kweli hayaji bila gharama kwa mazingira. Kwa hivyo, programu za urejeshaji wa mashimo, upandaji miti na elimu ya mazingira zinaendelea kupatiwa kipaumbele kikubwa.
Kwa kasi ya sasa, Ruangwa inajiandaa kuwa kitovu kikuu cha uwekezaji wa madini kusini mwa Tanzania. Sekta hii inabeba ahadi ya ajira, mapato, maendeleo, na hadhi mpya ya kiuchumi. Kutoka kwa vilindi vya mioyo ya viongozi na wananchi wa Ruangwa, tunawakaribisha wawekezaji wa sekta ya madini kwa mikono miwili.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa