
Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hassan Ngoma, amewaagiza wazazi na walezi kuhakikisha wanafunzi wote ambao bado hawajaripoti shuleni wanarejea mara moja kabla ya siku ya Jumatatu, akionya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaokaidi agizo hilo.
Agizo hilo limetolewa leo, tarehe 30 Januari 2026, wakati wa kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, kikiwahusisha Wakuu wa Idara na Vitengo, Maafisa Elimu wa Kata, Watendaji wa Kata na Vijiji na Kamati ya Ulinzi na usalama Wialaya, kwa lengo la kufanya tathmini ya mwenendo wa kuripoti shuleni na mahudhurio ya wanafunzi wa awali, msingi na sekondari.
Katika kikao hicho, Maafisa Elimu wamewasilisha taarifa kutoka kata zote 22, zikionesha idadi ya wanafunzi ambao bado hawajaripoti shuleni licha ya mwaka wa masomo kuanza.
Akizungumza baada ya kusikiliza taarifa hizo, Mhe. Ngoma amesema Serikali haitavumilia uzembe au kisingizio chochote kinachozuia watoto kupata haki yao ya msingi ya elimu. Amesisitiza kuwa elimu ni bure, hivyo hakuna sababu ya kuwazuia watoto kwenda shule.
“Nawagiza nyote kuhakikisha watoto ambao hawajaripoti shuleni wote wanaripoti. Hakikisheni wazazi wanawapeleka wote maana elimu ni bure. Asiwepo mtu wa kuleta kisingizio chochote. Siku ya Jumatatu ndiyo mwisho, wanafunzi wote waripoti shule walizopangiwa na kuandikishwa,” amesema Mhe. Ngoma.
Aidha, Mkuu wa Wilaya amesisitiza uadilifu kazini, kufanya kazi kwa bidii, kulinda taswira ya Serikali, kuepuka vitendo vya rushwa na propaganda zisizo za kweli, pamoja na kutenda haki kwa wananchi.
“Twendeni 2026 tukaichore taswira sahihi ya Serikali yetu, tukatoe huduma bora za kiuongozi kwa wananchi wetu. Kila mtu afanye kazi yake kwa usahihi ili tuone matokeo ya kazi zetu,” amesema.
Kikao hicho kimebainisha dhamira ya Serikali ya Wilaya ya Ruangwa kuhakikisha kila mtoto anapata elimu kwa wakati na kwamba ushirikiano wa wadau wote unahitajika ili kufanikisha azma hiyo.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa