Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Ruangwa limeendesha mafunzo ya kinga na tahadhari kwa watumishi wote wa makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, leo tarehe 15 Julai 2025. Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo kwa lengo la kuwajengea uelewa wa awali kuhusu namna ya kukabiliana na majanga kazini na majumbani.
Wakiendesha mafunzo hayo, SGT Richard Fredrick Urembo pamoja na FC Petro Simon Makalwe wamesema elimu hiyo imekusudiwa kuwapa watumishi maarifa ya kuzuia majanga kama moto, gesi na ajali za papo kwa papo. Aidha, wamefafanua kuwa hatua za haraka za awali huokoa maisha na mali kabla ya msaada wa kitaalamu kufika.
Kwa mujibu wa wawezeshaji hao, uelewa wa kinga dhidi ya majanga umebainika kuwa moja ya nguzo muhimu ya usalama kazini, wameeleza kuwa mara nyingi madhara makubwa hutokea kutokana na ukosefu wa maandalizi, vifaa sahihi au ujuzi wa kutumia njia salama wakati wa dharura.
Sambamba na hayo, watumishi wamefundishwa kwa usahihi namna ya kutumia kizimia moto, kufahamu aina mbalimbali za moto na namna ya kuuzima kulingana na chanzo chake. Pia, wameelekezwa hatua za msingi za kutoa msaada wa haraka kwa mtu aliyejeruhiwa katika tukio la moto au tukio la dharura.
Akizungumza kwa niaba ya Halmashauri, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Mhe. Adv. Zuberi Sarahani amepongeza Jeshi la Zimamoto kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo amesema yamewafumbua macho watumishi wengi kuhusu hatari walizokuwa hawazifikirii kila siku.
“Mafunzo haya yamekuwa msaada mkubwa, yameongeza uelewa wa tahadhari kwa mazingira yetu ya kazi na hata majumbani, ni matumaini yangu kuwa yataendelea kufanyika mara kwa mara kwa kuwa usalama ni jambo la msingi kwa maendeleo ya taasisi,” amesema Adv. Zuberi.
Mafunzo hayo yamehitimishwa kwa mazoezi ya vitendo ambapo watumishi wamejifunza namna ya kutumia kizimia moto (fire extinguisher), mbinu za kujiokoa na kuwasaidia wengine, ikiwa ni hatua ya kuimarisha usalama na utayari wao wa kukabiliana na majanga yanapojitokeza kwa ghafla katika mazingira ya kazi na nyumbani.
Kwa ujumla, mafunzo hayo yameongeza ari na uelewa miongoni mwa watumishi kuhusu wajibu wao katika kuhakikisha mazingira yao yanakuwa salama dhidi ya majanga. Halmashauri imedhamiria kuendelea kushirikiana na taasisi za uokoaji katika kujenga utamaduni wa tahadhari na uwajibikaji.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa