Zaidi ya Shilingi Milioni 565,517,154/= zimetolewa kwa vikundi 136 vya Wanawake, Vijana, na Watu wenye Ulemavu kupitia mpango wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, hafla ya uzinduzi wa mikopo hiyo imefanyika leo, Februari 7, 2025, katika ukumbi wa hoteli ya Ruangwa Pride, ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hassan Ngoma, kwa kushirikiana na uongozi wa Halmashauri hiyo.
Mhe. Ngoma ameagiza viongozi wa Wilaya na Halmashauri kuhakikisha kuwa kanuni za utoaji mikopo zinazingatiwa, mikopo inasambazwa kwa haki na kwa wakati, ili kufanikisha lengo la Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, la kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Ndugu Frank Komba, amesema kuwa kati ya vikundi vilivyonufaika, 78 ni vya Wanawake, 48 vya Vijana, na 10 vya Watu wenye Ulemavu. Ameeleza kuwa ufuatiliaji na usimamizi wa mikopo hiyo unapaswa kuimarishwa ili kuhakikisha marejesho yanafanyika kwa wakati na kuwapa fursa wengine kunufaika.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Andrew Chikongwe, amewataka wanufaika kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha wanarejesha kwa wakati, lakini pia, amesisitiza umuhimu wa wanavikundi kushiriki katika shughuli za kijamii na maendeleo, ikiwa ni pamoja na kuhudhuria mikutano ya hadhara.
Kwa upande wao, wanufaika wa mikopo hiyo, akiwemo Rehema Saidi, mwakilishi wa vikundi vya Wanawake, Kasimu Mnanguka kutoka Kikundi cha Mshikamano mwakilishi wa vijana, na Ramadhan Abdallah, mwakilishi wa Watu wenye Ulemavu, wameishukuru Serikali kwa kuwawezesha na wameahidi kurejesha mikopo kwa wakati ili kusaidia wengine kunufaika.
Ili kuhakikisha mpango huu unaleta matokeo chanya, ni muhimu kwa wanufaika kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuimarisha nidhamu ya marejesho.
@lindi-rs
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa