Wilaya ya Ruangwa imefanya bonanza la michezo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kilele cha maadhimisho ya Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara, ambayo Wilayani Ruangwa yatafanyika kesho tarehe 8 Desemba, bonanza hilo limefanyika leo tarehe 7 Desemba 2024, likihusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, rede, bao, na kuvuta kamba, kwa lengo la kuimarisha mshikamano wa kijamii na kusherehekea mafanikio ya Taifa.
Aidha, mashindano ya mpira wa miguu yamezua msisimko mkubwa, ambapo mchezo wa kwanza umezikutanisha timu za Kiwengwa na Ruangwa Boys, timu ya Kiwengwa imeibuka mshindi kwa mabao 3-1. Katika mchezo wa pili, Bodaboda kwa Wanyumbani imepoteza kwa mabao 5-2 dhidi ya Pachenga, hivyo basi timu za Kiwengwa na Pachenga zitakutana katika fainali, itakayofanyika kesho, tarehe 8 Desemba, katika viwanja vya Shule ya Msingi Likangara.
Hata hivyo, michezo mingine kama rede, bao, na kuvuta kamba nayo imefanyika kwa hamasa kubwa, washiriki na mashabiki wameshirikiana kuonyesha mshikamano, huku vikundi vya michezo vikifanya vizuri na kuvutia umati wa watazamaji.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Ruangwa, Ndugu Matiku Msonga, amesema kuwa bonanza hilo limeonesha ushirikiano wa hali ya juu miongoni mwa wananchi.
“Tunaendelea kuhimiza michezo kama sehemu ya kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuhamasisha uzalendo. Nawapongeza washiriki wote waliojitokeza kushiriki na kufanikisha tukio hili,” amesema Msonga.
Vile vile, maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu inayosema: “Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara – Uongozi Madhubuti na Ushirikishwaji wa Wananchi ni Msingi wa Maendeleo Yetu.”Kauli mbiu hii inahimiza mshikamano wa kitaifa na umuhimu wa kushirikiana katika maendeleo.
Ikumbukwe, Shughuli hizi zinaendelea kuleta hamasa kubwa kuelekea kilele cha sherehe za Uhuru, ambapo wakazi wa Wilaya ya Ruangwa wanatarajiwa kushiriki kwa wingi katika tukio hili la kihistoria.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa