Wenyeviti 525 wa Serikali za Mitaa, wakiwemo wenyeviti wa vijiji 90 na vitongoji 435, Wilayani Ruangwa wamepatiwa mafunzo ya uongozi leo, Desemba 19, 2024, mafunzo hayo yametolewa na wakufunzi kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa, Ombolo, Dodoma.
Mafunzo hayo yamefanyika katika bwalo la Shule ya Sekondari ya Wasichana Ruangwa, yakihusisha pia wakuu wa idara na vitengo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa.
Akizungumza kuhusu mafunzo hayo, kaimu Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu wa Halmashauri hiyo, ndugu Shadhili Msungu amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuwawezesha viongozi hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
“Lengo kuu ni kuwajengea uwezo wa kiuongozi ili waweze kusimamia maendeleo katika maeneo yao kwa misingi ya uwajibikaji na ushirikishwaji,” amesisitiza.
Miongoni mwa mada zilizojadiliwa ni pamoja na usimamizi wa miradi ya maendeleo, muundo wa Serikali za Mitaa, manunuzi ya umma, mawasiliano ya ufanisi, na utekelezaji wa sheria ndogondogo za Serikali za Mitaa.
Washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kufurahishwa kwao na hatua hiyo, wakisema itawasaidia kuimarisha uongozi na ushirikiano katika maeneo yao.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kuhakikisha viongozi wa ngazi ya msingi wanapata ujuzi unaohitajika kwa ajili ya maendeleo endelevu ya jamii.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa