Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ameendesha harambee na kuchangisha sh. milioni 928.67 za ujenzi wa kanisa kuu tarajiwa la Mt. Andrea Kagwa la Jimbo Katoliki la Lindi.
Kati ya fedha hizo, sh. milioni 464.3 ni fedha taslimu na nyingine kati ya hizo zimeshawekwa benki na sh. milioni 464.37 bado ni ahadi. Awamu ya kwanza ya ujenzi huo, inatarajiwa kugharimu sh. milioni 700.
Akizungumza na waumini na wadau mbalimbali waliohudhuria harambee iliyofanyika Ruangwa mjini, leo mchana (Jumamosi, Julai 27, 2024), Waziri Mkuu amewataka waliotoa ahadi wazikamilishe mapema ili kazi ya ujenzi isikwame.
"Ninawashukuru sana wote mliofika na wote waliochangia ujenzi wa kanisa tarajiwa. Ninawaomba walioahidi, wakamilishe ahadi zao mapema ili kazi ianze kwani ramani ipo, mafundi wapo tayari, wasimamizi wa ujenzi wapo," amesisitiza.
Waziri Mkuu amesema uamuzi wa Baba Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Mhashamu Askofu Wolfgang Pisa kuanza ujenzi wa kanisa kuu la jimbo hilo, ni utekelezaji wa maono aliyokuwa tangu aliposimikwa kuongoza jimbo hilo Juni, 2022.
"Mhashamu Baba Askofu Pisa ameanza kutekeleza maono yake kupitia kaulimbiu ya NINAONA KIU aliyoitangaza tarehe 26 Juni, 2022 wakati akisimikwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi. Ninawaomba wanaLindi tumpe ushirikiano kwa sababu maono yake ni endelevu. Ninawasihi tumpe ushirikiano ili aweze kutimiza hayo maono."
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi wazazi na walezi wawe karibu na watoto wao na wafuatilie hatua za ukuaji wao ili baadaye wawe raia wema.
Mapema, akisoma risala kuhusu mradi wa ujenzi wa kanisa tarajiwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Mhandisi Fortunatus Machibya alisema harambee hiyo imelenga kukusanya sh. milioni 900 ambapo kati ya hizo, sh. milioni 700 ni za ujenzi na sh. milioni 200 ni za maandalizi ya Jubilei ya miaka 25 ya upadrisho wa Askofu Pisa na miaka 50 ya Askofu Mstaafu wa Jimbo la Lindi, Mhashamu Askofu Bruno Ngonyani.
Alisema ujenzi wa kanisa hilo unahitajika kukamilika haraka kwa sababu wakati Jimbo Katoliki la Lindi linaanzishwa mwaka 1986, kanisa lililopo lilipewa tu hadhi na hapakuwa na kanisa jipya.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa