Baadhi ya wataalamu wa kilimo na mifugo pamoja na wajasiriamali kutoka Wilaya ya Ruangwa wamepatiwa elimu ya ujasiriamali na masoko katika maonesho ya Nanenane kanda ya kusini yanayoendelea kwenye viwanja vya Ngongo, Lindi Manispaa, Leo, tarehe 7 Agosti 2024.
Mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengea uwezo katika uendeshaji wa shughuli zao za kilimo na ufugaji kwa kutumia mbinu za kisasa za masoko na ujasiriamali, yametolewa kwenye banda la NMB Bank.
Aidha, Katika mafunzo hayo, wataalamu wamejifunza jinsi ya kuongeza thamani ya bidhaa za kilimo na mifugo kupitia usindikaji, ufugaji bora na mbinu za kisasa za kuhifadhi mazao. Hii itawawezesha kupata faida zaidi na kupunguza hasara zinazotokana na uharibifu wa mazao. Pia, wamepatiwa mbinu bora za utafutaji wa masoko na jinsi ya kutumia mitandao ya kijamii kama nyenzo muhimu ya kufikia masoko mapya na wateja wapya.
Vilevile, washiriki wameelimishwa kuhusu njia za kupata mikopo nafuu kutoka NMB Bank ili kuendeleza miradi yao ya kilimo na ufugaji. Hii ni pamoja na masharti rahisi na riba nafuu inayowezesha wakulima na wafugaji wadogo kupata mitaji ya kuendeleza shughuli zao. Uwezo wa kupata mikopo utasaidia kuboresha uzalishaji na kuongeza tija katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Katika hatua nyingine, wajasiriamali wamejifunza umuhimu wa kujiunga katika vikundi na ushirika ili kuweza kupata mafunzo zaidi na kujenga nguvu ya pamoja katika kusimamia masoko na kushiriki fursa za kibiashara. Ushirikiano huu unawawezesha kupata nafasi bora katika masoko na pia kushiriki kwenye maonesho na mafunzo mbalimbali yanayowapa maarifa na ujuzi zaidi.
Mafunzo ya namna hii ni muhimu sana kwa kuwa yanawawezesha wataalamu wa kilimo na mifugo pamoja na wajasiriamali kupata ujuzi na maarifa ya kisasa katika uendeshaji wa shughuli zao. Hii inawawezesha kuongeza uzalishaji, kupanua masoko na hatimaye kuboresha kipato chao na uchumi wa maeneo yao. Mafunzo haya pia yanachangia katika kuimarisha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini kwa ujumla.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa