Wanawake Wilayani Ruangwa Mkoani Lindi wametakiwa kuacha tabia ya kuwakatisha watoto ndoto zao hasa wanafunzi wa shule za msingi kwa kuwataka wajifelishe katika mitihani ya darasa la saba, kwa kigezo cha kutokuwa na uwezo wa kuwasomesha kujiunga elimu ya sekondari.
Hayo yamesemwa na Afisa wa kuzuia na kupambana na Rushwa Bi, Angela Mwabulambo alipozungumza mbele ya kina mama katika viwaja wa CWT Ruangwa wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, ambayo uadhimishwa duniani kote kila ifikapo machi 8.
Amesema Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa imekuwa na utaratibu kuandaa club za kupambana na rushwa kwa wanafunzi za msingi na sekondari, lengo kubwa likiwa ni kuwajenga watoto katika misingi ya uzalendo wa kuepuka na kukemea masuala ya rushwa jinsi yanavyopoteza haki.
“Tunapowahoji watoto na kutaka kujua sababu za wao kufanya vibaya katika mitihani yao wanafunzi wengi wameeleza kuwa wameambiwa na wazazi wao hasa kina mama kuwa wajifelishe kwani wao hawana uwezo wa kuwasomesha elimu ya juu” amesema Bi. Angela
Kutokana na taarifa hizo Bi, Angela amesema kufanya hivyo ni kumnyima mtoto haki yake ya msingi ya kupata elimu na kuwaomba wadau washirikiane kutolea taarifa matukio hayo katika vyombo vya sheria huku akiwahimiza wamama wapende watoto wao kwa kwa kuwapa elimu, kwani elimu ndiyo urithi pekee wa kueleweka kwa mtoto.
Wakati huo huo mlezi wa dawati la jinsia kutoka kituo cha polisi cha Ruangwa Afande Mpokigwa Mwamulanga amewataka wamama kufichua matukio ya unyanyasaji wanaotendewa kwa kutoa taarifa katika kituo cha polisi ili kutokomeza hali ya unyanyasaji wa kijinsia kwa kwa wanawake.
Aidha amesema matendo mengi yanafanyika ya kikatili kwa wanawake lakini kina mama wengi wamekuwa wakiyanyamazia na wengine hata kutokujua huku akitaja mifano ya matendo hayo kuwa pamoja na kupigwa, kutukanwa, kukashifiwa na kushikwashikwa sehemu yoyote ya mwili bila ridhaa.
Baadhi ya wanawake waliohudhuria wameeleza kuhusu kuhamasika kwao kushiriki katika shughuli mbalimbali za ujasilimiamali kama utengenezaji wa sabuni, batiki, ushonaji na kuwahimiza wanawake wengine kutobweteka katika shughuli kwani maendeleo hutokana na bidii ya kazi.
Kauli mbiu ya mwaka huu nchini Tanzania inasema kuelekea uchumi wa viwanda tuimarishe usawa, jinsia na uwekezaji wanawake vijijini, kauli hii inakuja ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano ya Tanzania ya viwanda.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa