Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hassan Ngoma, amewataka wananchi kutoingiwa na hofu watakapoona Kikosi Maalumu cha Kuzuia Ghasia (FFU) kikizunguka mitaani kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa, ameeleza kuwa kikosi hicho kitawasili wiki moja kabla ya uchaguzi kwa lengo la kuimarisha usalama katika Wilaya nzima ya Ruangwa.
Akizungumza leo, tarehe 7 Novemba 2024, katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Ngoma amesema kuwa hatua hiyo inalenga kutengeneza mazingira salama ya uchaguzi.
“Hakuna atakayepigwa, hakuna atakayefanywa chochote, Serikali inatumia gharama kubwa kwenye uchaguzi, hivyo ni lazima kuwepo na ulinzi wa kutosha kwa ajili ya wananchi,” amesema DC Ngoma.
Aidha, DC Ngoma amehimiza wananchi kuendelea na shughuli zao kwa amani, akisisitiza kuwa uwepo wa FFU ni wa kawaida na unalenga kuimarisha usalama, ameongeza kuwa Serikali ya Wilaya imejipanga kikamilifu kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa utulivu na amani.
Ikumbukwe kuwa usalama na amani ni muhimu katika kipindi cha uchaguzi ili kuwalinda wananchi na kuhakikisha mchakato mzima unafanyika bila vurugu. Mhe. Ngoma amesisitiza kuwa hali ya utulivu ni msingi wa maendeleo na mshikamano wa jamii, hivyo kila mmoja ana jukumu la kudumisha amani ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki na wa kuigwa duniani kote.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa