Katibu Tawala wa Wilaya ya Ruangwa, Mhandisi Zuhura Rashid, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, amezindua na kugawa miche ya minazi kwa wakulima kutoka kata 11 za Wilaya hiyo leo Januari 28, 2025, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kata zilizopokea miche hiyo ni Nkowe, Makanjiro, Malolo, Nandagala, Mandarawe, Mandawa, Mnacho, Chienjele, Ruangwa, Namichiga na Chibula. Zoezi hilo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuendeleza zao la minazi kama zao la biashara na chakula kwa Ukanda wa Pwani.
Kwa mujibu wa Mhandisi Zuhura, Wilaya ya Ruangwa imeanzisha kitalu chenye miche zaidi ya 4,000, huku tayari ikipokea miche 7,000 ya minazi ambayo imeanza kusambazwa kwa wakulima. Alisema kuwa upatikanaji wa miche hiyo ni sehemu ya ahadi ya Rais Samia aliyoitoa Septemba 18, 2023, alipofanya ziara mkoani Lindi na kuwaahidi wakulima miche 50,000 ya minazi.
“Aina ya miche tunayoigawa ni ya East Africa Tall (EAT) ambayo ni minazi mirefu ya asili, yenye uwezo wa kuzaa kati ya miaka mitano hadi saba, na kila mti unaweza kutoa zaidi ya nazi 45 kwa mwaka, pamoja na kustahimili magonjwa na wadudu kwa muda wa hadi miaka 70,” amesema Mhandisi Zuhura.
Aidha, ametoa wito kwa wakulima waliopokea miche hiyo kuhakikisha wanaifanya kuwa sehemu ya mapinduzi ya kilimo kwa kuitunza, kuilinda na kuikuza ili kufanikisha malengo ya Serikali katika kukuza kilimo cha minazi na kuongeza kipato cha kaya.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa