Wajumbe wa Serikali za Vijiji vya Kata ya Nandagala wamefanya sherehe ya kujipongeza kwa utumishi wao uliotukuka kwa kipindi cha miaka mitano tangu waingie madarakani. Sherehe hiyo imefanyika Agosti 12, 2024, katika bwalo la Chuo cha VETA Nandagala, kilichopo Kata ya Nandagala, Wilaya ya Ruangwa.
Sherehe hiyo iliyolenga kuwaaga Wajumbe hao kwa kipindi cha utumishi wao, imehudhuriwa na wageni mbalimbali kutoka Kata ya Nandagala, akiwemo Chifu wa Wilaya ya Ruangwa, Mzee Said Mohamed Chipenye, Mwenyekiti wa Wenyeviti Wilaya ya Ruangwa Mhe. Garus Nnunduma, na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa (Diwani wa Kata ya Nandagala) Mhe. Andrew Chikongwe, ambaye amekuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo.
Aidha, Wajumbe hao wametumia fursa hiyo kupongezana kwa mafanikio makubwa ya maendeleo waliyoleta ndani ya Kata yao katika kipindi cha miaka mitano ya utumishi wao, kuanzia mwaka 2019 hadi 2024. Wameeleza furaha yao kuwa sherehe hiyo imefana sana, huku wakiweka wazi kuwa ni mara ya kwanza kwa Wajumbe kujipongeza kwa utumishi bora ndani ya Kata ya Nandagala.
Mbali na hayo, Wataalamu wa Kilimo na Elimu wa kata hiyo wametoa shukrani zao kwa maendeleo makubwa yaliyopatikana katika sekta za Kilimo na Elimu, ikiwa ni pamoja na miradi mikubwa ya kilimo cha umwagiliaji na maendeleo ya elimu yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka mitano. Kwa moyo wa dhati, wameipongeza Serikali kwa juhudi zake za kuchapa kazi na kuleta maendeleo kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Garus Nnunduma, amewasisitiza Wajumbe wa Serikali za Vijiji kuzitendea haki nyadhifa walizopewa. Amesema, “Sherehe hii iwe chachu ya kujitathmini na kuzipima kazi mlizozifanya ndani ya miaka mitano, lakini pia iwaoneshe namna mnavyopaswa kuwajibika kwa ajili ya wananchi wenu. Ukipewa dhamana ya kuwatumikia wananchi, wajibika ipasavyo na siyo kuwa mtu wa kubisha na kupinga kila jambo.”
Naye, Chifu wa Wilaya ya Ruangwa, Mzee Said Mohamed Chipenye, amesema, “Uongozi bora unaanzia kwenye kujitambua na kuheshimu mila na desturi zetu, tunapoendelea na maendeleo ni muhimu kuhakikisha kwamba tunadumisha utamaduni wetu na kuendeleza maadili bora kwa kizazi kijacho.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa