Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hassan Ngoma, amewataka madiwani na viongozi wa vyama vya siasa kuzingatia amani na utulivu wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa, akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani leo, tarehe 7 Novemba 2024, Mhe. Ngoma amesema serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayekuwa chanzo cha taharuki au kuvuruga amani ya jamii.
Mhe. Ngoma ameeleza kuwa jukumu la viongozi ni kushiriki kuleta suluhisho la migogoro ili uchaguzi uwe wa haki na salama.
“Hatutaangalia chama, sheria itafuata mkondo wake kwa yeyote atakayevuruga amani,” amesisitiza Mhe. Ngoma.
Pia, Mhe. Ngoma amewakumbusha viongozi kuwa uchaguzi ni tukio la siku moja, hivyo waepuke kutengeneza uadui, chuki, na migawanyiko itakayodumu katika jamii, ameongeza kuwa Serikali ya Wilaya haitavumilia vitendo vya aina hiyo.
Katika kikao hicho, Katibu wa Waziri Mkuu Jimboni, Comredi Ramadhan Matola, ametoa wito kwa viongozi kutumia nafasi zao kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa ACT Wilaya ya Ruangwa, Ndugu Bakari Kungoni, amesisitiza umuhimu wa umoja ili kuleta mabadiliko chanya na kufanikisha Ruangwa kuwa mfano wa kuigwa.
Naye Mwenyekiti wa CUF, Ndugu Liwikila Mohamed (Obama), amehimiza utoaji wa elimu ya demokrasia kwa wananchi ili kuhakikisha uelewa mzuri kuhusu uchaguzi.
Ikumbukwe kuwa uchaguzi huu ni fursa muhimu kwa wananchi kuchagua viongozi watakaowawakilisha na kushughulikia changamoto zao, hivyo ni muhimu kuzingatia utulivu na mshikamano kwa ustawi wa jamii.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa