Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na taasisi za kifedha ikiwemo Benki Kuu, taasisi za uwekezaji na bima zimeshauriwa kuanzisha kliniki ya elimu ya fedha kipindi cha mavuno ili kuwafikia wakulima katika maeneo yao ya uzalishaji.
Ushauri huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, George Mbesigwe, alipokutana na timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha ambayo ipo mkoani humo kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali wakiwemo wakulima, wafanyabiashara na wanafunzi.
"Kipindi cha mavuno huku kwetu ndo kipindi ambacho wananchi wanakuwa na fedha, hivyo elimu hii ikitolewa wakati wa mavuno itasaidia wakulima kuhamasika kufungua akaunti benki, kufanya uwekezaji kupitia taasisi za uwekezaji au kukata bima ya mazao kwa kuwa zitakuwa zimefika katika eneo husika la mavuno," amesema Mbesigwe
Naye Afisa Maendeleo wa Wilaya ya Ruangwa, Edward Mbaruku ameahidi kuendelea kuwahamasisha wananchi wa halmashauri hiyo kujenga mazoea ya kujiwekea akiba, kukopa katika taasisi rasmi na hivyo kuepuka migogoro lakini pia kusajili vikundi ili waweze kutambulika na Serikali na kuwa na sifa ya kupata mikopo na fursa nyingine zinazotolewa kupitia vikundi.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa