Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa inashiriki Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini, yanayofanyika katika viwanja vya Ngongo vilivyopo Manispaa ya Lindi, maonesho yameanza rasmi tarehe 1 Agosti 2024 na kilele chake ni tarehe 8 Agosti 2024, ikumbukwe, manesho ya Nanenane yanatoa fursa kwa wananchi kujifunza na kuelewa teknolojia mpya zinazohusiana na kilimo, uvuvi, na ufugaji wa kisasa.
Hii ni fursa adhimu kwa wakulima, wafugaji, na wavuvi kuja kujifunza kuhusu mbinu bora na teknolojia za kisasa ambazo zinaweza kuboresha uzalishaji na kuongeza kipato. Huduma zitolewazo ni; Elimu ya upimaji afya ya udongo, Elimu ya matumizi bora ya mbolea, Elimu ya Mfumo wa M-KILIMO huu ni mfumo unaotoa huduma za ugani na masoko kupitia simu ya mkononi. Pia, maonesho haya yanatoa nafasi ya kuonyesha bidhaa mbalimbali na kujifunza kutoka kwa wataalam katika sekta husika.
Ikumbukwe, Maonesho ya Nanenane yalianza rasmi mwaka 1993 na yanaratibiwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Tukio hili la kitaifa linalenga kuhamasisha maendeleo katika sekta za kilimo, mifugo, na uvuvi. Kila mwaka, maonesho haya huandaliwa katika kanda tofauti nchini, ambapo wakulima na wadau wanapata nafasi ya kubadilishana uzoefu na kupata maarifa mapya. Maonesho haya yamekuwa yakifanyika kwa mafanikio na ni sehemu muhimu ya kalenda ya kilimo nchini.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni "Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi." Kauli mbiu hii inasisitiza umuhimu wa kuchagua viongozi wenye uwezo wa kuleta maendeleo endelevu katika sekta hizi muhimu za uchumi.
Tunawakaribisha kwa wingi kutembelea banda letu ili kupata maarifa muhimu ambayo yatasaidia kuboresha shughuli za uzalishaji. Pamoja, tutaweza kujifunza, kubadilishana mawazo, na kujadili mbinu bora za kuboresha ustawi wa jamii yetu. Karibu sana!
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa