Waziri wa Maji Nchini Prof. Makame Mbalawa ameagiza kusimamishwa kwa Mkandarasi anaeshughulika na ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Narungombe Wilayani Ruangwa Mkoani Lindi kutokana na mkandarasi huyo kutumia muda mrefu kutekeleza mradi huo ilhali alishalipwa awamu ya kwanza aliyostahili na kutakiwa kukamilisha mradi tokea mwezi februari mwaka huu.
Mhandisi huyo anaefahamika kwa jina la Waziri Jabiri wa kampuni ya SYSCON BUILDERS LTD, amechukuliwa hatua hiyo na prof. Mbalawa septemba 26 mwaka huu alipokuwa katika ziara yake ya kikazi Wilayani humo ambapo alifika katika kijiji cha Narungombe ambako kampuni hiyo ilipewa kandarasi kujenga mradi wa maji kijijini hapo kuonekana kutomaliza mradi kwa wakati licha ya mhandisi wa kampuni hiyo kukiri kupokea fedha za kazi hiyo na kutoitekeleza kwa wakati.
“kesho muanze taratibu za kumsimamisha Mhandisi huyo na mtupatie wenyewe tufanye kazi, hatuwezi kukaa na kuangalia wananchi wetu wanateseka na mimi siwezi kuja hapa kupiga maneno kila siku nikaonekana ni muongo, wakati naamini tukichukua sisi mradi ndani ya mwezi mmoja na nusu tunaumaliza kwa nini tukupe wewe wakati tushakupa muda na haukumaliza? ” alisema Prof. Mbalawa, alipokuwa akimhoji mhandisi Jabiri aliepewa kandarasi hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Rashidi Nakumbiya amepongeza maamuzi hayo ya Waziri kutokana na haja kuwa wananchi wamekua wakihitaji maji kwa muda mrefu bila mafanikio kutokana na uzembe wa mkandarasi huyo.
“haya malalamiko ya mradi kuchelewa wananchi wanayajua na wamelalamika kwa muda mrefu na wamepata hii tabu kwa muda mrefu, ilikua ndio kwa mara ya kwanza wenzetu hawa wapate maji lakini mwenzetu ambae alipaswa kushughulikia hili jambo ametuangusha hatua ulioichukua Mheshimiwa Mbalawa ni muafaka na kwa wakati muafaka ili kuweza kuokoa na kurudisha matumaini ya wananchi kwa serikali yao lakini pia kuondokana na tatizo la maji limekua ndoto zao kwa muda mrefu sana” alisema Mh. Nakumbya.
Baaadhi ya wananchi wakiwemo zaudia mjogo na Rashidi salumu wamesema wamekua wakipata tabu ya kujihimuu usiku wa saa tisa kufuata maji yaliko ili kuwahi foleni na wakati mwingine kupelekea kushinda huko siku nzima bila mafanikio na hivyo kusema kuwa kukamilika kwa mradi huo kunaweza kuja kuwakomboa na hadha hiyo ambayo wamekua wakiipata kwa miaka mingi sasa.
“tunashida ya maji hii tabu ni ya muda mrefu, tumeomba msaada toka muda mrefu, hatulali tunakesha maporini kwenye vyanzo vya maji kutafuta maji” alisema Zaudia majogo ambae ni mkazi wa Narungombe.
Mradi wa maji katika kijiji cha narungombe unagaharimu Shilingi milioni 300 huku zaidi ya milioni 100 zikiwa ameshalipwa mkandarasi huyo lakini bado utekelezaji wake umekua wa kusua sua jambo lilopelekea kusimamishwa kwa kandarasi yake.
MWISHO
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa