Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Kanda ya Kusini imeendesha mafunzo maalum kwa viongozi wa taasisi za umma, yakiwemo mashule na vituo vya afya, ili kuwajengea uwezo wa kutumia mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa ununuzi wa umma ujulikanao kama NeST.
Mafunzo hayo yamefanyika Aprili 14, 2025 katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Nkowe yamehusisha Waganga Wafawidhi, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu pamoja na Walimu wa Manunuzi, ambapo walifundishwa kuhusu matumizi sahihi ya mfumo huo kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 10 ya mwaka 2023 na Kanuni za mwaka 2024.
Akizungumza na washiriki, Afisa Manunuzi Mwandamizi wa PPRA Kanda ya Kusini, Mtaka Membe, amesema baadhi ya taasisi za umma katika ngazi ya msingi zimekuwa zikitumia fedha za serikali bila kufuata miongozo ya manunuzi, hali inayochangia kupotea kwa rasilimali na kuathiri uwajibikaji.
“NeST ni mfumo uliobuniwa kulinda fedha za umma kwa kuhakikisha uwazi, ushindani wa haki, na thamani halisi ya fedha katika kila hatua ya mchakato wa manunuzi,” amesema Membe wakati wa mafunzo hayo.
Taarifa kutoka PPRA zinaeleza kuwa mfumo wa NeST unajumuisha hatua zote kuanzia maandalizi ya mpango wa ununuzi, uandaaji na tathmini ya zabuni, utoaji wa tuzo, hadi usimamizi wa mikataba kwa njia ya kidijitali.
Mbali na hayo, washiriki walielimishwa kuhusu majukumu ya wadau mbalimbali wa manunuzi ndani ya taasisi zao, wakiwemo Maafisa Masuuli, Maafisa Manunuzi, Idara tumizi pamoja na Kamati za Zabuni ili kuhakikisha kila hatua ya ununuzi inatekelezwa kwa weledi.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo wamepongeza juhudi za PPRA, wakisema elimu waliyoipata itawasaidia kuboresha usimamizi wa rasilimali na kutumia mfumo wa NeST kwa ufanisi ili kuepuka ukiukwaji wa taratibu za kisheria.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa