Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula, ametembelea na kukagua kituo cha Askari wa uhifadhi wanyamapori leo Julai 17, 2024, kilichojengwa katika kijiji cha Machang’anja, Wilaya ya Ruangwa.
Kituo hicho kimejengwa kwa ajili ya kutoa msaada wa haraka kwa wananchi, ikiwemo kuimarisha ulinzi na kutoa elimu dhidi ya wanyama pori wanaovamia makazi ya watu, hususani tembo. Kituo kitahudumia Kata tatu zinazo kizunguka ambazo ni Makanjiro, Narungombe, na Mandawa.
Aidha, Mhe. Kitandula amezungumza na wananchi wa Kijiji cha Machang’anja, na amewahakikishia kuwa Serikali imejipanga vizuri kuleta suluhisho la kudumu kuhusu tatizo la tembo. Amewahimiza wananchi kutumia kituo hicho ipasavyo kwa kuwa kimejengwa kwa ajili ya kuwasaidia.
"Serikali imejipanga kununua helikopta mbili zitakazotumika katika zoezi la kuondoa tembo karibu na makazi ya watu. Kwa Wilaya ya Ruangwa, Serikali italeta mabomu 400 ya kufukuza tembo na kutoa mafunzo kwa vijana kuhusu namna ya kujilinda dhidi ya tembo. Pia, italeta mipira yenye kelele za kukera na vifaa maalum vya kutupa mabomu ili askari wasitumie mikono," alisema Mhe. Kitandula.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa