Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mhe. Andrew Chikongwe ametoa wito kwa Watendaji Kata, Watendaji wa Vijiji na Maafisa ugani kupambana na kuwajibika ipasavyo na kila mmoja kutimiza majukumu yake bila shuruti ili iwe chachu ya maendeleo katika Vijiji, Kata na Halmashauri kwa ujumla.
" Mabadiliko ni hatua, na hatua hiyo inahitaji utayari na uthubutu, endapo kila mmoja atatimiza wajibu wake kikamilifu tutapata hayo mabadiliko ya maendeleo katika vijiji vyetu, Kata zetu, na Halmashauri yetu"
Hayo ameyasema leo Juni 18, 2024 katika Kikao kazi kilichohusisha Watendaji Kata, Watendaji wa Vijiji, Maafisa ugani kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa.
Aidha Mhe. Chikongwe amewataka Maafisa ugani Kata kujua idadi kamili ya wakazi katika Kata husika ili kuweza kufanya hesabu ya kiasi gani cha chakula kinahitajika na hekari ngapi zinapaswa kulimwa ili kupata mazao ya chakula yanayokidhi mahitaji ya wakazi.
"Maafisa ugani hii ni kazi yenu, msisite kuwatembelea wakulima ili kuweza kuwafahamu kwa mmoja mmoja na kuwapa msaada wa kilimo bora cha kisasa kwa karibu kabisa kwa sababu hata hizo Korosho na Ufuta tunaoutegemea unalimwa na wananchi wa kawaida" Amesema Chikongwe.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa