Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mhe. Andrew Chikongwe amefanya ziara ya kuwatembelea wafugaji wa kuku kutoka kijiji cha Nandagala wilayani Ruangwa ambao ni wanufaika wa mradi wa TPGS akiambatana na Daktari wa Mifugo Kata ya Nandagala pamoja na Mtendaji Kata ya Nandagala.
Ziara hiyo ameifanya leo Julai 14, 2024 ikiwa na lengo la kutoa elimu kwa wanufaika wa mradi huo namna gani bora ya kufuga na faida zake na kutoa wito kwa wafugaji hao kuzingatia namna bora ya ufugaji kwani soko la kuku wa nyama na mayai halijawahi kujaa.
" Mimi niwaambie tu yakwamba hili jambo si dogo na lina manufaa makubwa sana kwenu, soko la kuku wa nyama na mayai halijawahi kujaa, wahitaji ni wengi sana endapo mutazingatia vizuri ufugaji huu, msidharau kabisa au kuishi kwa kitegemea kilimo tu hata ufugaji pia una manufaa kwetu" Amesema Chikongwe.
Mradi wa Tropical Poutry Genetics Solution (TPGS) una lengo la kuendeleza kizazi cha kuku na kuifundisha jamii namna gani nzuri ya kufuga kuku kwa maendeleo endelevu katika familia.
Ili kuendeleza kizazi cha kuku TPGS ina Kituo kikubwa cha chanjo za Mifugo ambapo kipo Arusha na kwa Kanda ya Kusini kipo kituo cha utafiti wa Mifugo Naliendele, Mtwara.
Kwa upande wao wafugaji wa kuku kutoka kijiji cha Nandagala walionufaika na Mradi huo, waliopata kuku 25 wapo nane, waliopata kuku 50 wapo nane na waliopata kuku 75 wapo nane na kufanya jumla ya watu 24 waliopatiwa kuku aina ya Saso na Tanbrow Juni 6, 2024.
Kuku aina ya Saso na Tanbrow wana uwezo wa kutaga mayai 270 - 300 kwa kila kuku mmoja kwa mwaka na ukomo wa kutaga mayai ni miaka miwili.
Kwa upande wake, Daktari wa Mifugo Kata ya Nandagala Jenifer Moses amesema ili kudumisha ufugaji wa kuku kuna haja ya kuwa na Kituo cha utafiti wilayani Ruangwa kwasababu itasaidia kupunguza gharama kwa mfugaji endapo mfugo utapata homa na kuhitajika kufanyiwa uchunguzi zaidi.
Naye, Mtendaji wa Kata ya Nandagala Bi Awesa Rashidi ametoa wito kwa wananchi kufuga kwa kuzingatia kanuni bora za ufugaji wa kuku na kuendeleza ufugaji huo kwani ni mtaji katika familia.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa