Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Hassan Ngoma ameongoza zoezi la upandaji miti kiwilaya lililofanyika leo Aprili 10, 2025 katika Shule ya Sekondari Kitandi iliyopo Kata ya Likunja, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Serikali inayolenga kila Wilaya kupanda miti.
Zoezi hilo limeratibiwa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kwa lengo la kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhifadhi mazingira, ambapo wananchi, walimu, wanafunzi na viongozi wa Serikali wameshiriki kikamilifu.
Akizungumza katika zoezi hilo, Mhe. Ngoma ametoa wito kwa walimu na wanafunzi wa shule hiyo kuitunza miti hiyo kwa uangalifu huku akiwasisitiza wafugaji kuhakikisha wanadhibiti mifugo yao kwa kufanya ufugaji wa zero grazing.
“Ni jukumu letu kuhakikisha miti hii inakua na kufanikisha lengo la Taifa la kuwa na mazingira bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema Mhe. Ngoma.
Kwa upande wake, Muhifadhi Misitu Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Bw. Samwel Tamka amewahamasisha wananchi kufika katika Ofisi za TFS kupata miche ya miti na kuipanda katika maeneo yao ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika utunzaji wa mazingira.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Kitandi, Mwl. Arafa Msuya ameushukuru Uongozi wa Wilaya pamoja na TFS kwa kuchagua shule yao kuwa sehemu ya zoezi hilo na kueleza kuwa miti hiyo itasaidia kupunguza mmomonyoko wa udongo unaosababishwa na mwinuko uliopo katika eneo la shule hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi, Hajra Selemani Hamis ameishukuru Serikali kwa zoezi hilo akieleza kuwa miti iliyopandwa itawasaidia wanafunzi kwa kutoa kivuli na kuboresha mazingira ya kujifunzia shuleni hapo.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa