Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Ndugu Frank Fabian Chonya, amewahimiza watumishi wa umma kufanya usafi wa mazingira na kushiriki mazoezi mara kwa mara ili kulinda na kuimarisha afya zao, akibainisha kuwa afya bora hujengwa kwa mtindo wa maisha unaozingatia usafi wa mazingira na mazoezi ya mwili.
Chonya ametoa wito huo leo Mei 10, 2025, mara baada ya kuongoza zoezi la usafi lililofanyika katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, likiwahusisha watumishi wa taasisi hiyo pamoja na vijana wa Skauti wa Wilaya ya Ruangwa ambao walishirikiana kusafisha maeneo ya ofisi na viunga vyake.
Aidha, Chonya amesema kuwa afya njema haihitaji dawa pekee, bali inahitaji utaratibu endelevu wa kufanya usafi, kufanya mazoezi, na kujali mazingira tunamoishi na kufanyia kazi.
“Watumishi wa umma wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa na jamii katika kulinda afya kwa njia ya vitendo” amesema Chonya.
Hata hivyo, zoezi hilo la usafi limelenga kuhamasisha utamaduni wa kufanya usafi wa mara kwa mara mahali pa kazi pamoja na kuamsha ari ya ushirikiano baina ya watumishi wa Serikali na makundi ya kijamii kama Skauti, ili kujenga jamii yenye afya, mshikamano na uwajibikaji wa pamoja.
Kwa upande mwingine, Afisa Elimu Msingi Mwl. George Mbesigwe akizungumza kwa niaba ya watumishi wa Halmashauri walioshiriki zoezi hilo amesema shughuli kama hizo zinapaswa kuendelea kufanyika mara kwa mara kwa kuwa huchangia kulinda mazingira, kuboresha afya ya akili na kupunguza msongo wa mawazo kazini.
Sambamba na hayo, kiongozi wa vijana wa Skauti Wilaya ameleza kuwa ushiriki wao haukuwa tu wa kimwili bali pia wa kihisia, kwani umewapa nafasi ya kujenga mahusiano mema na wenzao, huku wakihisi kuwa sehemu ya jamii inayojali afya na ustawi wa pamoja.
Halikadhalika, Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa imekuwa ikiendeleza kampeni ya usafi na mazoezi kwa watumishi wake kama sehemu ya utekelezaji wa sera ya afya kazini, sambamba na kuunga mkono juhudi za kitaifa za kuimarisha afya ya jamii kupitia mabadiliko ya tabia na mazingira ya kazi.
Ikumbukwe, juhudi hizi ni sehemu ya dhamira pana ya kuhakikisha Tanzania inakuwa taifa lenye afya bora, mazingira safi na jamii inayowajibika, ambapo taasisi za umma zinakuwa kinara katika kuhamasisha mabadiliko chanya kwa vitendo.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa