Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Ndugu Frank Fabian Chonya, amefanya kikao na watumishi wote wa Makao Makuu ya Halmashauri hiyo kwa lengo la kujadili masuala ya kiutumishi na kuimarisha uwajibikaji kazini.
Kikao hicho kimefanyika leo Julai 25, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri na kimekusudia kuweka misingi bora ya utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia maadili ya kazi, weledi na nidhamu kwa kila mtumishi wa umma.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Chonya amesisitiza kwamba kila mtumishi anatakiwa kuwajibika ipasavyo ili kufanikisha maendeleo ya Wilaya ya Ruangwa na taifa kwa ujumla. Amesema nidhamu na uaminifu kazini ni misingi muhimu ya mafanikio ya taasisi yoyote.
Aidha, amewataka watumishi wote kuendeleza ushirikiano waliouonesha katika kipindi kilichopita, hali ambayo imesababisha Halmashauri hiyo kufanikisha ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 101 katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Pamoja na hayo, Mkurugenzi amesisitiza kuwa mafanikio hayo yanapaswa kuwa chachu ya kuendeleza bidii na kujituma ili makusanyo ya mapato kwa mwaka wa fedha 2025/2026 yawe bora zaidi.
Vilevile, amewaasa watumishi kuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wananchi kwa uadilifu na kwa kuzingatia dira ya maendeleo ya Wilaya, huku akiwataka kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya mahali pa kazi.
Kwa upande wao, watumishi wa Halmashauri hiyo wamemshukuru Mkurugenzi kwa uongozi wake bora, ushirikiano na moyo wa kujali ustawi wa watumishi, na wameahidi kuendelea kutoa huduma kwa weledi na uadilifu kwa maendeleo ya Ruangwa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa