Katika maandalizi ya kushiriki mashindano ya SHIMISEMITA 2025 yatakayofanyika Agosti Jijini Tanga, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Ndugu Frank Fabian Chonya, amekabidhi vifaa vya michezo kwa timu ya watumishi wa Halmashauri hiyo, leo Julai 23, 2025.
Makabidhiano hayo yamefanyika katika Uwanja wa Majaliwa ambapo Mkurugenzi Chonya amesema lengo ni kuhamasisha afya, mshikamano na ushiriki wa watumishi katika shughuli za kitaifa.
Akizungumza katika hafla hiyo fupi, Chonya amesema kuwa vifaa hivyo ni motisha kwa wachezaji, lakini zaidi ni wito wa ushindi na uwakilishi wa heshima kwa Ruangwa.
“Mkiwa wawakilishi wa Ruangwa, tunatarajia mkaoneshe nidhamu, ushindani na uzalendo. Sisi ni timu moja ndani na nje ya kazi,” amesema Chonya.
Kwa kuongezea, vifaa vilivyotolewa ni pamoja na seti mbili za jezi rasmi, soksi, mipira ya mazoezi, vihuzi na vifaa vingine muhimu kwa maandalizi ya timu.
Aidha, amekumbusha kuwa wachezaji hao wanabeba taswira ya Halmashauri wanaposhiriki mashindano ya SHIMISEMITA, hivyo wanapaswa kuwa mfano wa nidhamu na mshikamano hata nje ya uwanja.
Kwa upande mwingine, watumishi walioshiriki hafla hiyo wameeleza kufurahishwa kwao na hatua hiyo, wakisema imeongeza ari, mshikamano na morali kuelekea mashindano hayo ya kitaifa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa