Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mhe. Andrew Chikongwe ametoa wito kwa Taasisi ya fedha, Benki ya NMB tawi la Ruangwa kumwezesha mkulima katika nyenzo kwani mkulima akikwamuliwa basi inasaidia hata Benki hiyo kujikwamua kiuchumi.
"Watu wapo tayari kwa kilimo, lakini wanakosa nyenzo, hivyo basi nikuombe Meneja wa Benki ya NMB kuwasaidia wakulima hawa kupata nyenzo zitakazowasaidia kuongeza kasi ya uzalishaji na wewe ni mwenzetu na tuna imani kubwa sana na wewe ya kwamba utatukwamua katika hili" Amesema Chikongwe.
Ameyasema hayo leo Julai 12, 2024 katika Kikao kilichofanyika katika Kijiji cha Namahema B kilichopo Kata ya Nandagala wilayani Ruangwa.
Kikao hicho kilihusisha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Viongozi wa Kata ya Nandagala, Viongozi wa kijiji cha Namahema B, Viongozi wa Benki ya NMB, na wakulima wa bustani za mbogamboga wa Kata ya Nandagala na Mnacho.
Pia, Kikao kilihusisha kutembelea wakulima wa bustani za mbogamboga akiwemo Ndugu Mohamed Said Chipenya ambaye anajihusisha na kilimo hicho kwa umwagiliaji wa mkono (mashilingwete), Imamu Abeid pamoja na Mussa Nassoro ambao hutumia njia za kisasa katika kilimo hicho cha mbogamboga na kuona utofauti mkubwa uliopo kati ya mkulima ambaye hutumia njia zisizo za kisasa na yule ambaye hutumia njia za kisasa katika kilimo hicho.
Kwa upande wake Meneja wa Benki ya NMB tawi la Ruangwa Ndugu Habibu Moris amesema nia wanayo ya kuwasaidia wakulima kwa sababu kupitia ziara ya kuwatembelea wakulima wamejifunza mengi lakini uaminifu ni silaha kubwa sana katika kufanikisha hayo yote.
" Ni kweli mkulima akikwamuliwa na sisi tunakuwa tumejikwamua kwasababu Benki kazi yake ni kuhifadhi akiba za watu, na kutoa mikopo kwa watu, hivyo tunavyoamua kuwakopesha na nyie muoneshe uaminifu kwa kurejesha mikopo kwa wakati ili kuendelea kufanya kazi kwa weredi kama Taasisi, usivyorudisha kwa wakati wengine wanakosa huduma" Amesema Moris
Kijiji cha Namahema B kina jumla ya wakulima 215 ambapo wakulima wa mbogamboga ni 86, wakulima wa Korosho ni 40 na wakulima wa mazao ya chakula ni 89.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa