Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ruangwa Rashidi Nakumbya amewataka wahudumu wa afya kufanya hamasa kwa wamama wajawazito ili waweze kuingizwa katika mpango wa tumaini la mama.
Alisema kufanya hivyo itasaidia sana kupunguza idadi ya vifo vya wakina mama na watoto wachanga kwani watakuwa wamepata huduma mapema na mtoto ataendelea kupata huduma bora na bure kwa muda wote wa ujauzito.
Aliyasema hayo wakati akiongea na wahudumu wa afya waliohudhuria kwenye mafunzo yaliyotolewa na Ofisi ya Bima ya Afya Mkoa, alitumia nafasi hiyo kuishukuru Ofisi ya Bima ya Afya Mkoa na Benki ya serikali ya Ujerumani.
Aidha Mhe. Nakumbya aliwaasa wahudumu wa afya kuwa na lugha nzuri za kuzungumza na wateja pale wanapoitaji huduma, kwani hii itasaidia kuwepo na ukaribu wa mgonjwa na mtoa hudumu.
Mhe. Mwenyekiti alisema kuwa kuna changamoto nyingi ambazo watumishi wa afya hukutana nazo maeneo yao ya kazi, hata hivyo hawapaswi kukata tamaa bali kuzifanya changamoto hizo kuwa ni fursa ili kufikia malengo mazuri ya kumaliza vifo vya watoto na wazazi.
Naye Meneja wa Mfuko wa Bima ya Afya Mkoa Bwana Emmanuel, Mwikwabe alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwasaidia watanzania kupata huduma za afya kwa urahisi kupitia bima, alisisitiza gharama za matibabu ni kubwa bila bima ya afya ni vingumu kila mwananchi kupata huduma anazoziitaji.
Aliwataka wahudumu wa afya kujitahidi kutumia nafasi hii iliyopatikana kuwasajili akinamama kwa wingi na kutoa elimu ya bima ya afya kwa wateja wao, ikitokea jamii ikatambua umuhimu wa bima ya afya wananchi watapiga hatua katika maendeleo ya jamii.
Naye Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Japhet Simeo aliwataka watumishi wa afya kuwatumia wahudumu wa afya kwa ngazi ya vijiji kwani wao ni rahisi kuwabaini akina mama wajawazito kwenye maeneo yao.
Tumaini la mama ni fao linalotolewa na Mfuko wa Bima ya Afya.Fao hili linafadhiliwa na benki ya wananchi wa ujerumani, lengo kuu la fao hili ni kuboresha afya ya mama mjamzito na miezi 6 baada ya kujifungua. Pia kuboresha upatikanaji wa dawa,vitendanishi na vifaa tiba. Halikadhalika Fao hili litasaidia kuboresha Miundombinu ya kutolea huduma
Tumaini la mama ni fao ambalo mama yoyote mjamzito husajiliwa na kupewa namba ya utambulisho ambayo huandikwa kwenye kadi yake ya kliniki na kumruhusu kutibiwa mahali popote ndani ya Mkoa
Vile vile fao limetoa fursa ya kuwalipia kadi za (CHF) wanafamilia wa mama wajawazito kwa mwaka mmoja, wanufaika hawa wa CHF hutibiwa ndani ya Halmashauri husika.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa