Waziri Mkuu na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, Mhe. Kassim Majaliwa, amesema Wilaya ya Ruangwa imenufaika kwa kiasi kikubwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza leo Mei 3, 2025, katika kikao cha wajumbe wa mabaraza ya Jumuiya za CCM kilichofanyika katika bwalo la Shule ya Awali na Msingi ya Wonder Kids, Majaliwa amesema kuwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia, miradi mikubwa imeanzishwa na mingine kuendelea kutekelezwa kwa mafanikio makubwa.
Aidha, Katika sekta ya afya, amesema idadi ya vituo vya afya imeongezeka kutoka viwili mwaka 2010 hadi kufikia 12, huku zahanati zikiongezeka kutoka 22 hadi 35, hatua iliyosogeza huduma karibu na wananchi na kupunguza msongamano katika hospitali kubwa.
Ameongeza kuwa, Sekta ya elimu pia imenufaika kwa kiasi kikubwa ambapo shule za sekondari zimeongezeka kutoka 16 hadi 30, jambo lililosaidia kuongeza fursa za elimu kwa watoto wa Ruangwa na kupunguza umbali wa kutafuta shule.
Sambamba na hayo, Waziri Mkuu ameeleza kuwa mradi mkubwa wa maji wa Nyangao–Ruangwa–Nachingwea unaendelea kutekelezwa, ukihusisha vijiji 34 vya Ruangwa na vijiji 21 vya Nachingwea, na unatarajiwa kuwahudumia wakazi 128,657 baada ya kukamilika.
Wilaya hiyo inaendelea na ujenzi wa barabara za ndani kwa kiwango cha lami pamoja na ujenzi wa barabara ya Nanganga–Ruangwa ambayo ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji, ikilenga kuboresha usafiri na uchukuzi ndani ya Wilaya.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hassan Ngoma, ameipongeza Serikali kwa kufanikisha utekelezaji wa miradi hiyo na kusisitiza kuwa Serikali inaendelea kujidhatiti kuboresha huduma muhimu za kijamii kwa wananchi wa Ruangwa.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa