Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Andrew Chikongwe, amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kuendeleza utamaduni wa kufanya usafi wa mazingira, kuwekeza katika kilimo cha kisasa, na kujali afya zao, akisema afya bora ni msingi wa maendeleo ya mtu binafsi na jamii kwa ujumla.
Wito huo umetolewa leo Aprili 16, 2025, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Mbekenyera, ambapo viongozi mbalimbali wa kata, wajumbe wa Serikali za Vijiji, vikundi vya wanufaika wa mikopo, pamoja na wananchi wamehudhuria na kujadili namna ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.
Aidha, Mhe. Chikongwe amesema maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila wananchi kuwa na afya njema, mazingira safi na kushiriki kwenye shughuli za uzalishaji mali kama kilimo.
“Tukijenga haya matatu kwa pamoja usafi wa mazingira, kilimo cha kisasa na afya bora tutakuwa tumejenga msingi wa maendeleo endelevu,” amesema Mhe. Chikongwe.
Sambamba na hayo, ametoa wito kwa wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kuhakikisha wanazitumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kujikwamua kiuchumi, akisisitiza kwamba Fedha hizo si kwa matumizi binafsi wala za anasa, bali ni mtaji wa maendeleo, wazitumie kwa umakini ili zitengeneze matokeo chanya.
Katika hatua nyingine, amewahimiza wazazi kuwa na ushirikiano wa karibu na walimu kwa kufuatilia maendeleo ya watoto wao badala ya kuwaachia walimu jukumu hilo pekee. “Wazazi mnapaswa kushirikiana na walimu ili kuhakikisha watoto wetu wanafanya vizuri. Malezi na elimu ni jukumu la pamoja,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mbekenyera, Mhe. Hamis Chimale, ameunga mkono kauli hiyo ya Mwenyekiti na kuwataka wananchi kuyafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa ili kuleta maendeleo kwa wote.
Naye Mohammed Kassim, ambaye amezungumza kwa niaba ya wananchi waliohudhuria mkutano huo, ameushukuru uongozi wa Halmashauri kwa kuandaa mkutano na kutoa elimu kwa jamii.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa