Mwenyekiti wa Halmashauri, Mheshimiwa Rashidi Nakumbya ameiagiza serikali ya Kijiji cha Mitope kuwachukulia hatua wafugaji wa ng’ombe wa maziwa wanaouza ng’ombe waliopata kupitia mradi wa kopa ng’ombe lipa ng’ombe.
Pia aliitaka Serikali ya Kijiji kuwachukulia hatua wafugaji wanaochinja ng’ombe hao badala ya kuendeleza mradi huo kwani kufanya hivyo ni kuhujumu mradi huo ambapo inapelekea kupoteza sifa za kupata tena mikopo hiyo.
Mheshimiwa Nakumbya, aliyasema hayo wakati wa ziara ya Kamati ya Ujenzi, Uchumi na Mazingira ilipofanya ziara yake ya robo ya kwanza ya kutembelea miradi ya maendeleo inayoendelea katika Wilaya ya Ruangwa.
Mhe Nakumbya aliutaka uongozi wa kijiji hicho kuandaa sheria ndogo zitakazowabana hao wafugaji wanaouza na kuchinja hao ng’ombe, pia alikiagiza kikundi cha wafugaji kufanya marekebisho ya katiba yao ili watu wasiwe wanauza na kuchinja mifugo ovyo.
“Kiukweli nimefarijika sana kukuta huu mradi katika kijiji cha Mitope kwani sehemu nyingine walishauza na kuchinja mifugo yote nitashirikiana na nyie bega kwa bega kuendeleza hiyo mifugo”alisema Nakumbya.
Naye Mhe Diwani wa kata ya Mbwemkuru aliwataka wanakikundi kurekebisha mabanda wanayolaza mifugo yao kwani mifugo hiyo ndiyo inayowaingizia kipato ni wajibu wakaithamini.
“Nyie mnaishi katika majumba mazuri ambayo yametokana na faida ya ng’ombe hao halafu hao wanaowapa hayo mafanikio hamuwajali si uungwana rekebisheni mabanda msimu wa mvua unakuja wajengeeni mabanda ya kudumu yaliyoezekwa juu.
Wakati huo huo kamati ilifanya Ziara katika mabonde yanayolimwa kilimo cha mbogamboga, bonde la Likunja, Mnindu na Chikalala ambapo wanakamati walipata fursa ya kuonana na wanavikundi na wakulima mmoja mmoja wanaojishughulisha na kilimo cha mbogamboga.
Mhe, Mwenyekiti aliwataka wakulima kuunda umoja wa AMCOS wa wakulima wa mbogamboga ambao utawasaidia katika masuala ya mauzo ya bidhaa hizo wanazolima.
“Undeni AMCOS ambayo itakuwa na katiba na miongozo mchague viongozi wenu watakaowasimamia katika kuendesha chama hicho mkifanya hivi hamtokuwa mnatoa changamoto ya ukosefu wa masoko ya kuaminika.
Pia aliwataka kutunza mazingira ya maeneo ya mabonde hayo ili vyanzo vya maji visikauke, aliwataka wapande miti ya kutosha kuzunguka vyanzo vya maji hivyo na kufuata sheria ya kuwa mbali na chanzo cha maji kwa mita 60.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa