Maonesho ya 31 ya Nanenane Kanda ya Kusini yametamatika leo 8 Agosti 2024 kwa mafanikio makubwa, yakionesha maendeleo ya sekta ya kilimo, ufugaji, na uvuvi katika Mikoa ya Lindi na Mtwara. Maonesho hayo, ambayo yamefanyika kwa siku nane katika viwanja vya Ngongo, Lindi, yamehudhuriwa na maelfu ya wakulima, wafugaji, wavuvi, na wadau mbalimbali kutoka maeneo mbalimbali ya kanda ya kusini na nje ya kanda hiyo.
Katika hotuba yake ya kufunga maonesho hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais ,Ikulu (kazi maalum), Mhe. George H. Mkuchika, amepongeza jitihada za wakulima na wadau wa sekta ya kilimo katika kuongeza uzalishaji na ubunifu. Amesema maonesho ya mwaka huu yameweka rekodi mpya kwa kuonesha teknolojia za kisasa zaidi zinazoweza kuboresha uzalishaji na kuongeza tija katika sekta ya kilimo.
Aidha, Mhe. Mkuchika amewaimiza wakulima kufanya shughuli zao za kilimo kwa bidii maana kilimo ni uti wa mgongo amewaomba kutumia vizuri elimu walizopatiwa kwenye maonesho ya 31 ya Nanenane kanda ya kusini 2024 ili kufanya kilimo chenye tija na manufaa kwao na kwa Taifa kwa ujumla.
Sambamba na hayo, Mhe. Mkuchika amesisitiza Wananchi wote wenye sifa kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa lakini pia, wasiache kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, ili waweze kutimiza takwa lao la kikatiba la kuchagua viongozi wao.
Mbali na hayo, zawadi kwa makundi mbalimbali yaliyofanya vizuri zimetolewa kwenye maonesho hayo ikiwa ni sehemu ya motisha na kujali juhudi na jitihada za wadau wa kilimo, mifugo na uvuvi.
Ikumbukwe, Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, kujifunza teknolojia mpya, na kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya kilimo, ufugaji, na uvuvi. Serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha kuwa maonesho haya yanaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa kanda ya kusini na Tanzania kwa ujumla. Mwaka ujao, maonesho haya yanatarajiwa kuwa na mwitikio mkubwa zaidi, huku serikali ikiahidi kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika sekta ya kilimo na ufugaji.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa