Wizara ya Katiba na Sheria imefanya kikao kazi na wataalamu kuelekea uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika Mkoa wa Lindi, Kikao hicho kimefanyika leo Februari 18, 2025, katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, kikiwaleta pamoja Maafisa Maendeleo ya Jamii, Maafisa Ustawi wa Jamii, Wanasheria, Maafisa Habari, Wapima Ardhi, Wasajili na Polisi kutoka Dawati la Jinsia.
Kampeni hiyo inalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao za kisheria na kuwapatia msaada wa sheria bure, hususan kwa wanawake, watoto, na makundi mengine yenye uhitaji na inatarajiwa kusaidia kutatua migogoro ya ardhi, ndoa, mirathi, na masuala mengine ya haki za binadamu, huku ikitekelezwa katika Mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa awamu.
Aidha, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Nathalis Linuma, ambaye amefungua kikao kazi hicho, amesema wataalamu wa sheria wanapaswa kushirikiana kwa karibu na jamii ili kuhakikisha elimu ya msaada wa kisheria inawafikia wananchi wengi zaidi kwa wakati muafaka.
Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Esther Msambazi, amesema uzinduzi rasmi wa kampeni hiyo utafanyika Februari 19, 2025, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa.
Ameongeza kuwa kampeni hiyo tayari imefika katika mikoa 17 na imeonyesha mafanikio makubwa kwa kuwawezesha wananchi kupata msaada wa kisheria na kutatua migogoro mbalimbali. Malengo ya kampeni hiyo ni kufikia mikoa 26 ya Tanzania Bara na mikoa 5 ya Zanzibar ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wananufaika na huduma hizo.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Ardhi, Andrew Munisi, amesema watahakikisha wananchi wanapata msaada wa kisheria katika utatuzi wa migogoro ya ardhi, huku Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Lindi, Joyce Kitesho, akisisitiza kuwa kampeni hiyo ni nyenzo muhimu ya kusaidia wanawake na watoto waliokumbwa na changamoto za kisheria.
Kwa miaka ya nyuma, wananchi wengi wamekuwa na uelewa mdogo kuhusu haki zao za kisheria, hali iliyopelekea ongezeko la migogoro na manyanyaso, hata hivyo, kupitia kampeni hii, Serikali imeongeza mwamko wa wananchi juu ya haki zao. Hatua inayofuata ni kuhakikisha elimu hii inawafikia wananchi wengi zaidi kwa wakati sahihi.
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imebeba kauli mbiu “Msaada wa Kisheria kwa Haki, Usawa, Amani na Maendeleo,”
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa