Maafisa maendeleo ya jamii ngazi ya kata wamepewa mafunzo kuhusu usimamizi na utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana, na walemavu mafunzo hayo yamefanyika leo, Oktoba 1, 2024, katika ukumbi wa Ofisi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa.
Mafunzo hayo yamehusisha maafisa maendeleo ya jamii kutoka kata zote 22 za Wilaya ya Ruangwa yakiwa na lengo la kuimarisha uelewa kuhusu mikakati ya usimamizi wa maendeleo ya jamii, hususani katika kusimamia mikopo ya 10% kwa kufuata taratibu zote zinazotakiwa.
Aidha, mafunzo yameendeshwa na Maafisa maendeleo ya Jamii ngazi ya Wilaya wakiongozwa na ndugu Rashid Namkulala, ambaye ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ruangwa, ambapo Ndugu Namkulala amesisitiza umuhimu wa mikopo hiyo katika kuboresha maisha ya wanajamii, huku akiwataka maafisa hao kuyazingatia mafunzo ili kuboresha zaidi utenda kazi wao katika kusimamia mikopo hiyo.
"Mikopo hii inatoa fursa kwa vikundi vya wanawake, vijana, na walemavu kujiendeleza kiuchumi na hivyo kuchangia katika maendeleo ya jamii nzima, ni matumaini yangu kwamba mafunzo haya wataongeza mara dufu utenda kazi wenu na pia yatasaidia kuleta mabadiliko chanya." Amesema Namkulala.
Sambamba na hayo, mafunzo hayo yameletwa wakati ambapo kuna umuhimu mkubwa wa kuimarisha ushirikiano kati ya Halmashauri na vikundi vya maendeleo. Washiriki wamepata nafasi ya kujifunza kuhusu taratibu za kuandika maombi ya mikopo, pamoja na jinsi ya kusimamia fedha hizo kwa ufanisi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa, hii inatarajiwa kuongeza ufanisi katika matumizi ya rasilimali.
Mbali na hayo, katika kipindi cha mafunzo, washiriki wamehusishwa moja kwa moja katika mijadala, ambapo wameweza kutoa mawazo na maswali kuhusu usimamizi wa mikopo hiyo, pia yametoa fursa ya kubadilishana uzoefu na kukuza mbinu bora za kazi.
Ikumbukwe, Maafisa maendeleo ya jamii wamehimizwa kuendeleza elimu waliyoipata kwa vikundi vyao ili kuhakikisha rasilimali zinatumika ipasavyo na kusaidia katika kuboresha maisha ya jamii. Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa inaamini kuwa mafunzo hayo yatakuwa chachu ya mabadiliko chanya katika maendeleo ya jamii.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa