Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi ameitisha kikao cha wadau wa elimu wilaya ya Ruangwa ili kujadili namna gani wilaya inapanda kiufaulu kwa mitihani ya taifa ya shule za msingi na sekondari tofauti na hali mbaya ya ufaulu iliyopo sasa.
Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa Narung’ombe uliopo Ruangwa mjini na uliwashirikisha Walimu, wenyeviti wa kamati na bodi za shule, maafisa elimu kata, madiwani, wenyeviti wa vijiji, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, wazee maarufu na wazazi.
Mhe. Zambi alisema kuwa mkoa kiufaulu upo chini sana ambapo kwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana ulikuwa wa 27 na kwa upande wa shule za msingi ulikuwa wa 14.
Katika majadiliano mdau wa Elimu Mheshimiwa Diwani Elias Nkane alisema ni lazima kuwe na ushirikiano baina ya walimu na waratibu elimu, madiwani, wazazi na viongozi wote katika wilaya katika kusimamia maendeleo ya elimu.
Aidha, Damares Namlehu alisema kumekuwa na tabia ya baadhi wazazi kutekeleza watoto wao bila sababu za msingi ambapo ameiomba serikali kuwachukulia hatua wazazi wenye tabia hizi na wale wanaofanya kilimo cha kuhamahama ambacho kinapelekea utoro mashuleni.
Naye Issa Mmaka amesema tatizo jingine ni ukosefe wa walimu wa sayansi na hisabati katika shule na kusababisha watoto kufanya vibaya kwenye mitihani ya masomo hayo.
Chilemba Daniel amesema maafisa elimu msingi na sekondari wapite katika kila shule kufuatilia mara kwa mara maendeleo ya wanafunzi na walimu. Pia alishauri lugha ya kingereza ufundishwaji wake usimamiwe kuanzia darasa la tatu.
Naye Hassan Snola amesema wazazi wanatakiwa kuacha kuingilia majukumu ya walimu kwani kwa kufanya hivyo kunasababisha walimu kukatatamaa na kushindwa kufanya kazi kama inavyotakiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Mhe. Joseph Mkirikiti amewataka watu kuacha kukaa vijiweni, maana wanafunzi wanaotoroka shule wanaenda kwenye vijiwe hivyo kuanzia sasa kutakuwa na operationi maalamu ya watu wanaokaa vijiweni.
“Niwaagize watendaji wa kata na vijiji kuanzia kesho kupita katika vijiwe, vibanda vya sinema na maeneo mengine kuwakamata watoto watoro na kuhakikisha mnawachukulia hatua kali wamiliki wa vibanda vya video wanao waruhusu wanafunzi kuingia humo badala ya kusoma”, amesema Mhe. Mkirikiti.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa alishauri wazazi kupitia kamati na bodi za shule kuona umuhimu wa kuchangia chakula katika shule kwa kufuata utaratibu ili kuondoa changamoto iliyopo ya watoto kukaa na njaa muda mrefu hali inayoondoa usikivu wa masomo ipasavyo.
“Suala la kuchangia chakula ni hiyari ya mzazi halazimiswi ila sisi kama serikali tunawaeleza umuhimu wa chakula kwa wanafunzi wanapokuwa shuleni na nimeshaelekeza kuwa mwanafunzi ambaye mzazi wake ataki kuchangia chakula asifukuzwe badala yake ukifika muda wa chakula huyo mtoto asipewe chakula.”, amesema Mhe. Zambi.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa