Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Ndugu Frank Fabian Chonya amefungua Kikao cha mrejesho cha Timu ya Usimamizi wa Huduma za Afya Mkoa wa Lindi (RHMT) kilichofanyika leo tarehe 19 Juni 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo.
Katika kikao hicho, Dkt. John Sijaona amewasilisha mrejesho kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi, ambapo ameeleza tathmini ya hali ya utoaji huduma za afya wilayani Ruangwa. Dkt. Sijaona amepongeza maboresho ya mazingira katika vituo vya kutolea huduma za afya, akiutaja kuwa ni mfano wa kuigwa miongoni mwa Wilaya za Mkoa wa Lindi.
Aidha, amewataka viongozi wa afya wilayani hapo kuhakikisha mapungufu yote yaliyoainishwa katika taarifa hiyo yanashughulikiwa kikamilifu kabla ya ukaguzi ujao.
“Tujipange kuhakikisha changamoto zilizobainika hazijirudii katika tathmini inayofuata,” amesema Dkt. Sijaona.
Vilevile, kikao hicho kimehudhuriwa na Madaktari na Waganga Wafawidhi wa vituo vyote vya kutolea huduma za afya, Wakuu wa Idara na Vitengo (CMT), wajumbe wa Timu ya Usimamizi wa Huduma za Afya ngazi ya Mkoa (RHMT), pamoja na wajumbe wa Timu ya Usimamizi wa Huduma za Afya ngazi ya Wilaya (CHMT).
Kwa ujumla, lengo la kikao hichi ni kupokea na kujadili mrejesho wa tathmini ya utoaji wa huduma za afya katika Wilaya ya Ruangwa, kama ilivyofanywa na Timu ya Usimamizi wa Huduma za Afya Mkoa wa Lindi (RHMT).
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa