Wananchi wa Kijiji cha Namilema, Kata ya Mbekenyera, Wilaya ya Ruangwa, wamepata elimu ya masuala ya kisheria kupitia kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, iliyofanyika leo, Februari 25, 2025, katika viwanja vya Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji.
Elimu hiyo imetolewa ili kuwawezesha wananchi kufahamu haki zao za kisheria, ikiwa ni pamoja na masuala ya mirathi, haki za watoto, ndoa, na talaka. Viongozi wa kampeni hiyo wameeleza kuwa lengo ni kuwajengea wananchi uelewa wa sheria na kuwasaidia kupata huduma za msaada wa kisheria wanapokumbana na changamoto mbalimbali.
Akizungumza katika kampeni hiyo, Antony Elias ambaye ni mratibu wakampeni ya mama Samia Legal Aid wilayani Ruangwa amesema watoto wana haki ya kuendelea kuwa na mahusiano na wazazi wote wawili hata baada ya wazazi kutengana, jambo linaloendana na sheria za haki za mtoto nchini.
Kwa upande wao, wananchi walioshiriki kampeni hiyo wameeleza kufurahishwa na elimu waliyopata, wakisema itawasaidia kufanya maamuzi sahihi wanapokutana na changamoto za kisheria katika maisha yao ya kila siku. Wametoa pongezi kwa Serikali kwa kuanzisha kampeni hiyo ambayo inaleta manufaa makubwa kwa jamii.
Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa na lengo la kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya kisheria na huduma za msaada wa kisheria kwa urahisi.
Ruangwa
Anuani ya Posta: S.L.P 51
Simu ya Mkononi: 0732932312
simu: 0732932312
Barua pepe: ded@ruangwadc.go.tz
Hatimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa